Askofu Amani awataka mapadri, watawa kuchukua tahadhari ya corona

Askofu Amani awataka mapadri, watawa kuchukua tahadhari ya corona

Muktasari:

  • Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani ametoa waraka akiwataka waumini kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Covid-19 ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maelezo kuwa ugonjwa huo bado upo na unayasumbua mataifa mbalimbali duniani.

Arusha. Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani ametoa waraka akiwataka waumini kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Covid-19 ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maelezo kuwa ugonjwa huo bado upo na unayasumbua mataifa mbalimbali duniani.

Katika waraka huo kwenda kwa mapadri, watawa na walei wa jimbo hilo aliouita ‘kutembea pekupeku juu ya mbigili’, amesema baada ya kutangazwa kuwa ugonjwa huo haupo nchini, watu wameacha kuchukua tahadhari.

"Maji ya kunawa mikono yameondolewa kanisani na mahala pengine yapo, lakini watu  hawanawi tena kwa imani kwamba hakuna corona, ile tahadhali ya kujikinga wameiacha na bado wanashikana mikono,” amesema huku akigusia utaratibu wa utoaji sadaka na kukomunika.

Amesema mapadri na watawa walihimizwa kuwa waangalifu zaidi ili wasisababishe maambukizi miongoni mwao na wanaowahudumia, “ilihimizwa pia kuvaa barakoa kwenye vyombo vya usafiri wa watu wengi, sokoni, kwenye ibada na hospitali.”

"Kutokana na hali halisi  inapaswa kujenga utamaduni na tabia mpya za kujinusuru kwa vingine kwa hakika tunatembea sasa  pekupeku juu ya mbigiri, tutafakari hali halisi kwani mwenye macho haambiwi tazama,” amesisitiza.

Amebainisha kuwa lengo la waraka wake ni  kumwalika kila mtu ajisimamie kwa usalama wake binafsi na kujali usalama wa wengine kwani Corona inatikisa ulimwengu, “na sisi tusijidanganye kiasi cha kutochukua tahadhari.”

"Tusimjaribu Mungu kwakufanya uzembe na afya zetu, Turejee tahadhari za kuzuia maambukizi bila kuwa na hofu, hakuna haja ya kufungiwa, tuendelee kusali na kuchukua tahadhali. Ukiona unawashwa kwenye koo, kukauka koo kikohozi kikavu, joto kubwa na kupumua kwa taabu haraka mwone daktari ili usaidiwe." alisema