Askofu Mengele amtetea Askofu mwenzake mgogoro KKKT

Askofu Mengele amtetea Askofu mwenzake mgogoro KKKT

Muktasari:

  • Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjilisti la Kirutheri Tanzania (KKKT), Isaya Mengele ameingilia kati mgogoro baina ya waumini wa kanisa hilo dayosisi ya Tukuyu Wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya wanaomtuhumu Askofu wa kanisa hilo, Dk Edward Mwaikali kuchukua mali za kanisa kinyume cha utaratibu.

Mbeya. Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjilisti la Kirutheri Tanzania (KKKT), Isaya Mengele ameingilia kati mgogoro baina ya waumini wa kanisa hilo dayosisi ya Tukuyu Wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya wanaomtuhumu Askofu wa kanisa hilo, Dk Edward Mwaikali kuchukua mali za kanisa kinyume cha utaratibu.

Dk Mwaikali anadaiwa kuhamishia mali hizo katika Makao Makuu ya Dayosisi ya Ruanda Jijini hapa.


Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 27, Mengele amesema kuwa uamuzi wa kuhamisha mali za kanisa  kutoka dayosisi ya Tukuyu ulipitishwa kwenye kikao  na halmashauri kuu na hizo tuhuma hizo siyo za kweli.


"Uamuzi wa kuhamisha  mali ni uamuzi wa vikao vya Halmashauri Kuu ya Kanisa na mimi kama Askofu mwazilishi, nalibariki suala hilo na ninatoa  maagizo kwa uogozi wa kanisa kukaa na waumini wa Dayosisi ya Tukuyu kumaliza tofauti zao zinazochoche migogoro," amesema.


Amesema awali kabla ya kumaliza muda wake suala hilo  lilikuwa tayari limepitishwa, ila muda wa kuhamisha mali ulikuwa bado, hivyo kitendo cha kumtuhumu na kuleta mogogoro kwa Askofu Mwaikali sio cha kiungwana na chukizo kwa Mungu.


"Tumefika na Mbeya na baadhi ya viongozi kuja kujiridhisha na taratibu zote zimefuatwa hivyo tumelibariki. Lengo ni kusogeza huduma mkoani.


“Hata ukiangalia taasisi za serikali zipo hapa mkoani, iweje kanisa likakae vijijini huko Tukuyu?" amehoji.


Kwa upande wake Askofu Dk Edward Mwaikali, alisema amesikitishwa na kitendo alichofanyiwa, kutukanwa na kufedheheshwa kwani suala la kuhamisha mali ni vikao vilikaliwa na halmashauri na sio mimi.


"Sio mimi niliyefanya uamuzi, waumini viongozi wa kanisa wakiwepo wachungaji tulipaswa kukaa mezani kuelekezana na kulimaliza na si kufikia hatua ime ambayo ilishtua umma wa watanzania" amesema.


Awali Agosti 22, mwaka huu katika Kanisa la KKKT dayosisi ya Konde Tukuyu waumini wa kanisa hilo walifanya vurugu kwenye ibada kupinga Askofu Mwaikali kuhamishia mali za kanisa katika makao makuu ya Kanisa la Ruanda Jijini hapa jambo lililosababisha Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumtoa Askofu huyo ndani ya kanisa.


Miongoni mwa sababu zikizosababisha waumini kufanya vurugu ni pamoja na kumtuhumu kuhamisha mali za kanisa, matumizi mabaya ya madaraka na kuwatimua kazi wachungaji 17 waliokuwa wakimshauri.