Askofu Niwemugizi: Mwalimu Nyerere angekuwepo, angecharaza watu viboko

Askofu Niwemugizi: Mwalimu Nyerere angekuwepo, angecharaza watu viboko

Muktasari:

  • “Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Julius Kambarage) angekuwepo na kushuhudia yanayotokea nchini kwa sasa angepasuka moyo, angepiga watu viboko hadharani na pengine angemwomba Mungu aichukue roho yake kama alivyofanya Nabii Musa nikitumia mfano wa maandiko ya Biblia Takatifu.”


“Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Julius Kambarage) angekuwepo na kushuhudia yanayotokea nchini kwa sasa angepasuka moyo, angepiga watu viboko hadharani na pengine angemwomba Mungu aichukue roho yake kama alivyofanya Nabii Musa nikitumia mfano wa maandiko ya Biblia Takatifu.”

Hiyo ni kauli ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi akizungumzia miaka 22 ya kifo cha Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Kiongozi huyo wa kiroho anasema Mwalimu Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza alikokuwa anatibiwa, angekuwa hai hadi leo, angewaadhibu hadharani baadhi ya viongozi kuanzia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi serikalini kutokana na mmomonyoko wa maadili.

“Uadilifu wa baadhi ya viongozi waliokabidhiwa dhamana ya ofisi za umma unatiliwa mashaka sana ndiyo maana matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma umekuwa jambo la kawaida. Tumemsikia Rais Samia Suluhu Hassan akitishia kuonyesha rangi zake halisi iwapo fedha za kukabiliana na athari za Uviko-19 zitatumika vibaya,” anasema.

Huku akichukua tahadhari kwa kuchagua maneno na hoja zake, Askofu Niwemugizi anataja baadhi ya maeneo anayoamini yangemsononesha Mwalimu Nyerere iwapo angekuwa hai hadi leo kuwa ni kummonyoka kwa maadili ya uongozi, kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali na fedha za umma, ubinafsi na matumizi mabaya ya madaraka na ofisi.

Askofu Niwemugizi: Mwalimu Nyerere angekuwepo, angecharaza watu viboko

“Siyo kwamba hakukuwa na tuhuma au vitendo vya rushwa wakati wa Mwalimu Nyerere. Vilikuwepo. Lakini viongozi wa wakati ule waliposema wanachukia rushwa ilionekana kweli wanaichukia kwa maneno na matendo vyao tofauti na sasa ambapo kuchukia rushwa imekuwa suala la maneno bila vitendo,” anasema.

Kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja, anasema Mwalimu Nyerere angefanya kila njia kusahihisha mambo ndani ya CCM ambacho ndicho kinaongoza dola na iwapo ingeshindikana, angetoka hadharani kukosoa na kutoa mwongozo, pengine kujitoa CCM.

“Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa uhuru wa mawazo, mijadala na kujenga hoja. Alipenda kuona jamii ya watu wanajadiliana kwa hoja hata pale wanapokinzani kimtazamo. Hakupenda hoja za upande mmoja ndiyo maana licha ya wenzake ndani ya CCM kupinga mfumo wa vyama vingi, yeye alishauri uruhusiwe,” anasema Askofu Niwemugizi.

Anasema hali imebadilika siku hizi ambapo hoja hazijibiwi kwa hoja imara na bora zaidi, bali nguvu na mamlaka ya dola.

“Hoja za upande wa upinzani zikionekana kuwa na nguvu, basi nguvu ya dola hutumika kuzizima huku mwenye maoni tofauti na utawala akionekana kuwa siyo mzalendo. Mwalimu Nyerere alikuwa tayari kusikiliza maoni ya wengine hata kama hakubaliani nayo na kuyajibu kwa hoja,” anasema.

Anasema siyo ajabu hivi sasa kuona vyombo vya dola vikitumika kuzima fikra, mawazo na sauti za watu wenye mawazo kinzani na yale ya mfumo wa uongozi na kuna hisia inaanza kujengeka ndani ya jamii kuwa kuna upendeleowa haki za kisiasa na kiraia ambapo walioko nje ya mfumo wa utawala wanazuiwa kusema au kufanya ambayo walioko ndani wanafanya.

“Nchi yetu inaongozwa katika misingi ya sheria lakini wakati mwingine sheria zinatungwa kuyalenga makundi ya watu badala ya maslahi ya Taifa. Ndiyo maana si ajabu kuwasikia baadhi ya waliohusika kutunga sheria wakizishangaa sheria walizozitunga,” anasema kiongozi huyo wa kiroho.

Ujamaa

Akizungumzia ujenzi wa Taifa na jamii moja, Askofu Niwemugizi anasema hadi mauti yanamfika, Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa Azimio la Arusha kwa sababu lilijikita katika misingi ya haki, undugu, utaifa, usawa na maendeleo endelevu kwa wote.

“Imani ya ujamaa alioupigania Mwalimu haupo tena, iliuwawa angali yuko hai. Kila mtu sasa hivi anajiangalia nafsi yake. Lakini yeye, hadi mauti aliamini katika misingi ya utu, usawa na haki ndiyo maana alisema anatembea na vitabu viwili pekee; Biblia na cha Azimio la Arusha,” alisema.

Katiba Mpya

Akizungumzia vuguvugu la madai ya Katiba Mpya, kiongozi huyo anasema Mwalimu Nyerere angekuwepo angeunga mkono wazo la Taifa kupata Katiba Mpya inayoweka miongozo mizuri ya uongozi na kuunda taasisi imara zisizotegemea uwezo na utashi wa mtu binafsi.

“Katiba bora huzaa sheria nzuri, zinazoweka miongozo na dira huku ikiwabana wanaokabidhiwa dhamana ya uongozi bila kutegemea utashi binafsi kwa sababu itaunda taasisi imara zinazosimamia masuala yote ikiwamo nidhamu na maadili ya viongozi,” anasema Askofu Niwemugizi.

Anasema Katiba bora itaweka mfumo na mipaka ya madarakaka kwa viongozi na kutoa uhakika wa utawala bora, utu, usawa na haki ya kila mtu.

Wanasheria

Akizungumzia demokrasia, utawala wa sheria, Katiba Mpya na miaka 22 ya kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere, kiongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kanda ya ziwa, Lenin Njau anasema si jambo baya kuwa na vuguvugu la kudai Katiba Mpya japo ni muhimu umma uijue Katiba ya sasa, ubora, uimara na udhaifu.

“Watanzania wakijua ubora, uimara na udhaifu wa Katiba ya sasa ndipo wataamua ni maeneo gani ya kurekebisha. Kwa maoni yangu, wengi bado hawaijui vema hata iliyopo hivyo kuna hatari ya tupigania mabadiliko yanayosukumwa na kundi la wenye nia ya kugawana madaraka,” anasema Njau.

Akitaja baadhi ya maeneo anayoamini yanahitaji marekebisho, wakili huyo anasema “nafasi za kiutendaji wakiwamo makatibu wakuu wa wizara, wakurugenzi na wakuu wa taasisi za umma zisiwe za uteuzi bali zitangazwe na kushindaniwa kwa sifa na vigezo. Wanaofanikiwa wapewe malengo na kupimwa kwa matokeo.”

Kuhusu ubunge na uwaziri, kwa maoni yake, Njau anasema tunapoadhimisha miaka 22 ya kifo cha Mwalimu Nyerere tufikirie kuwa na Katiba inayoweka mfumo unaotenganisha nafasi za ubunge na uwaziri.

Anasema wabunge wasalie kuwa wawakilishi na watetezi wa wananchi huku wakiisimamia Serikali huku mawaziri ambao watapatikana nje ya Bunge wakisimamia utekelezaji wa sera, maelekezo na mapendekezo ya wananchi kupitia kwa wabunge wao.

“Mfumo huu utaondoa migongano ya kimaslahi kati ya nafasi ya ubunge na uwaziri,” anasema wakili Njau.