ATCL kuanza safari ya China Machi 20

Muktasari:

  • Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) imesema kuanzia Machi 20, 2021 itaanza kufanya safari kati ya Dar es Salaam na Guangzhou, China.

Dar es Salaam. Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) imesema kuanzia Machi 20, 2021 itaanza kufanya safari kati ya Dar es Salaam na Guangzhou, China.

Itatumia ndege kubwa aina ya B787-800 Dreamliner zenye uwezo wa kusafiri takribani saa 11, amesema mkurugenzi mtendaji wa ATCL,  Ladislaus Matindi na kubainisha kuwa wanaoruhusiwa  kwenda China ni raia wa nchi hiyo na wasafiri wenye shughuli maalumu.

"Safari zetu zitafanyika kila siku ya Jumamosi, ndege itaondoka Dar es Salaam saa 11 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki na kuwasili Guangzhou  saa tatu usiku kwa saa za China siku hiyohiyo kisha kuondoka China  saa tano na kuwasili Dar es Salaam Jumapili saa 11 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki," amesema Matindi.

Amesema serikali ya China imeweka masharti na utaratibu wa kufuata ambapo kila msafiri anatakiwa kuzingatia.

"Utaratibu uliopo kwa sasa ni kwamba kila anayekwenda China anatakiwa kupima vipimo viwili vya ugonjwa wa Covid-19 ndani ya saa 48.”

"Endapo msafiri hatakuwa na maambukizi au viashiria vya maambukizi, basi atapewa vyeti viwili kutoka maabara kuu ya Taifa vinavyoonesha kuwa hana maambukizi au viashiria vyovyote vya ugonjwa wa Covid-19,” amesema Matindi.

Amesema baada ya kupata vyeti hivyo, mhusika atakwenda ubalozini kupata viza  na kibali maalumu Green health code kinachomruhusu kuingia nchini China.

“Baada ya kukamilisha taratibu hizo zote ndipo ATCL inaweza kumsafirisha kwenda nchini China.  Kwa wasafiri wanaotoka China kuja nchini hakuna masharti zaidi ya yaliyotangazwa na wizara ya afya,” amesisitiza.