ATCL yasitisha safari za India

Tuesday May 04 2021
atclpic

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limetangaza kusitisha safari zake kwenda nchini India ambako vifo na maambukizo ya corona yanazidi kuongezeka.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi mtendaji na ofisa mtendaji mkuu wa shirika hilo, Ladislaus Matindi inasema safari hizo zimesitishwa kuanzia leo, Mei 4.

“ATCL itaondoa faini zote kutokana namabadiliko haya, itatoa tiketi nyingine au kuwarudishia nauli zao abiria waliokuwa wamekata tiketi,” amesema Matindi.

Ili kupata ufafanuzi zaidi, Matindi amewataka abiria waliokata tiketi kupiga namba O800110045 bure.

Taarifa nchini India zinasema leo pekee, maambukizo mapya 357,229 na kufanya jumla kuwa zaidi ya milioni mbili. Kwa idadi hiyo, India inakuwa miongoni mwa mataifa yenye maambukizo mengi zaidi duniani.

Mpaka sasa ni Marekani pekee yenye idadi kubwa, zaidi ya maambukizo milioni tatu yaliyotokea kabla ya kuanza kutolewa kwa chanjo na Brazil inashika nafasi ya tatu ikiwa na zaidi ya maambukizo milioni 1.5 yaliyothibitika.

Advertisement

Mpaka sasa, Serikali ya India imeshatoa chanjo kwa zaidi ya watu milioni 16.69 bure huku dozi milioni 7.5 zikiwa zinaendelea kutolewa. Taifa hilo lenye watu bilioni 1.4 ni la pili kwa idadi kubwa duniani likiwa nyuma ya China.


Advertisement