Athari wazee kushiriki ngono na wasichana

Athari wazee kushiriki ngono na wasichana

Muktasari:

  • Wakati tabia ya wazee kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana wadogo ikianza kuota mizizi kwenye jamii na kuonekana jambo la kawaida, wataalamu wameeleza kuwa kuna athari nyingi za kiafya kwa mwanamume kuliko faida anazoweza kupata.

Dar es Salaam. Wakati tabia ya wazee kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana wadogo ikianza kuota mizizi kwenye jamii na kuonekana jambo la kawaida, wataalamu wameeleza kuwa kuna athari nyingi za kiafya kwa mwanamume kuliko faida anazoweza kupata.

Siku za karibuni kumekuwepo matukio ya wanaume kufia kwenye nyumba za wageni na baadaye inakuja kubainika kuwa alikuwa na binti mdogo. Wapo pia wanaobainika kuwa vifo vyao vimechangiwa na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu na uwezo wa kufanya tendo la ndoa.

Mwananchi imefuatilia undani wa suala hili na kuzungumza na wataalamu walioeleza athari zake kiafya na kijamii.


Kwa nini uhusiano huu?

Akizungumza na gazeti hili, mkazi wa Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam, Jane Sanga alisema wanaume wenye umri mkubwa mara nyingi si wasumbufu kwenye mahusiano ikilinganishwa na vijana.

Kando na hilo, alisema wanaume hao sio wagumu kutoa fedha kuwahudumia wenza wao, kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kwa sasa ndiyo kinaendesha mahusiano.

“Ukweli ni kuwa watu wazima sio wasumbufu katika mapenzi, tofauti na vijana ambao kila siku ugomvi mara wivu ili mradi mikwaruzano, lakini ukipata mtu mzima maisha yanakwenda vizuri.

“Ukiacha suala la utulivu, watu wazima sio wagumu kutoa hela, pale unapomwambia shida yako anakuwa tayari kukusaidia, kwani yeye anachohitaji ni mapenzi tu,” alisema Jane.

Naye Miriam Msonde alisema wanaume wenye umri mkubwa wengi wanakuwa na familia zao, hivyo muda mwingi hutumia huko, hali inayomfanya binti kuwa huru.

“Wasichana wengi siku hizi hatupendi kubanwa, hivyo ukiwa na mzee wako maisha yanakuwa freshi kabisa usiku anakuwa kwa mkewe na wewe unaendelea na ustaarabu mwingine, ila jambo la muhimu hawa wanatoa sana hela,” alisema Miriam.

Wakati wanawake wakisema hivyo, wanaume wamekuwa na mtazamo tofauti wakieleza kwamba, kikubwa wanachohitaji kwa mabinti wadogo ni kukidhi mahitaji yao ya kimwili.

John Ndumbaro (62) alieleza kuwa wanaume wengi wanatoka nje ya ndoa zao na kutafuta mabinti wadogo kwa kuwa wanawajali kuliko wake zao.

“Ukikaa na mwanamke miaka mingi mnazoeana hata yale mapenzi hayawi kama awali, ndio maana wengi wanaona watafute mbadala nje na huko huwezi kuchukua mtu mzima mwenzio, lazima upate damu changa.

“Hawa watoto wadogo wanajali mno, wako vizuri katika mapenzi na kwa kuwa ni vijana, utundu unakuwa mwingi, vitu ambavyo haviwezi kupatikana nyumbani, ndio maana mtu unakuwa tayari kwa lolote,” alisema.

Mwingine ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake alisema: “Kadiri mwanamke anavyozidi kuwa mkubwa uwezo wake wa kushiriki tendo la ndoa unapungua na inaweza ikatokea hivyo wakati mumewe bado ana nguvu, ndipo hapo mtu unaona upate kibinti chako maisha yaende.

“Halafu suala la kufurahia mapenzi kwa kiasi kikubwa ni mwanamume ndio maana anakuwa tayari kutumia chochote kuhakikisha anamudu tendo na ndio maana sio ajabu kusikia hizi dawa za kuongeza nguvu.”

Mwanasaikolojia Eliezer Lyimo amesema kadri umri unavyozidi kusonga binadamu anatakiwa kubadilisha mifumo ya maisha, ikiwemo matumizi ya nguvu na hata mpangilio wa vyakula, na hii ni kutokana na matatizo mbalimbali ya uzee.

“Wazee wengi wana changamoto za kiafya, hata uwezo wa kufanya tendo la ndoa unapungua, kuna mabadiliko ya kisaikolojia yanatokea, ule uwezo na kasi aliyokuwa nayo wakati wa ujana inapungua, sasa asipoelewa ndio atataka kushindana,” alisema.

Alisema kuwa wanaume wengi wanapokuwa na mafanikio, hasa ya kifedha wanaamini wanaweza kufanya vitu hasa wasivyoweza kufanya na mwisho wa siku huishia kujiingiza kwenye mahusiano hayo.

“Ikitokea siku zote hakuwa na uwezo wa kupata binti sasa amepata mafao yake kitu cha kwanza anachoweza kuwaza ni kutimiza haja yake bila kujali umri, mwingine ni changamoto za ndoa anatafuta watu wa kupoteza naye muda,” alisema Lyimo.


Kiafya hili likoje

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa wanaume, Steven Kaali alisema tendo la ndoa linahusisha moyo na kadiri umri unavyosogea kiungo hicho kinakuwa dhaifu, hivyo ni hatari kukutana kimwili na mtu ambaye moyo wake unasukuma damu kwa kasi.

“Tendo la ndoa kwa mwanamume linashikilia uhai, moyo unahusika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa ndio unasukuma damu inayosababisha uume usimame.

“Hata wakati wa kufanya tendo hilo moyo unafanya kazi, sasa umri unavyokwenda uwezo wa moyo kufanya kazi unapungua na ikitokea amekutana na binti mdogo ambaye mwili wake uko vizuri anaweza akamsabibishia msisimko utakaompa shambulio la moyo,” alisema.

Dk Kaali alisema hatari hutokea zaidi pale mwanamume anapotumia dawa za kumuongezea uwezo wa kushiriki tendo hili.

“Hizi dawa zina athari moja kwa moja kwenye moyo, anapozitumia analazimisha mwili kufanya kazi ambayo haina uwezo kwa wakati huo, hivyo kujikuta akipata shinikizo la damu na ndiyo tunasikia watu wanafia kwenye nyumba za wageni,” alisema Dk Kaali.

Kwa upande wake, Mfamasia na mkufunzi wa shule ya Famasia katika Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba alisema inapotokea mtu mzima anatumia dawa za kumuongezea uwezo wa kushiriki tendo la ndoa, kuna uwezekano wa kupata shida kiafya.

Akifafanua kuhusu dawa, hasa ikiwemo ile maarufu ya Viagra na nyingine, zikiwemo za mitishamba ambazo zinatumika kuongeza uwezo wa kufanya mapenzi, alisema zina uwezo wa kushusha shinikizo la damu na mwili hivyo kusababisha moyo kupiga kwa kasi.

“Hizi dawa kitabibu ikiwemo Viagra hapo awali zilikuwa zinatumika kushusha presha ya mapafu, sasa kama mtu anatumia kwa kiwango kikubwa na hana tatizo hilo basi upo uwezekano wa presha ya mapafu kushuka.

“Si hivyo tu, inaongeza kasi ya upumuaji, mtu anaweza kukosa oksijeni katika baadhi ya viungo, ikiwemo ubongo, figo, ini na hapo anaweza kupata shambulio la moyo na kusababisha kifo cha ghafla,” alisema Myemba.