Aunty Ezekiel ajifungua mtoto wa kiume

Aunty Ezekiel ajifungua mtoto wa kiume

Muktasari:

Mwigizaji wa Tanzania, Aunty Ezekiel amejifungua mtoto wa kiume jana Ijumaa Novemba 17,  2020 na kumpa jina la Noman.

Dar es Salaam. Mwigizaji wa Tanzania, Aunty Ezekiel amejifungua mtoto wa kiume jana Ijumaa Novemba 17,  2020 na kumpa jina la Noman.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Aunty (34) alichapisha video inayomuonyesha akiwa kwenye hospitali huku akimbembeleza mtoto huyo kwa kumuimbia wimbo wa “Nibakishie” wa wanamuziki Nandy na Alikiba na kuambatanisha maneno haya, “asante Mungu kwa zawadi.”

Noman anakuwa  mtoto wa pili kwa Aunty kwani mwaka 2015 staa huyo ambaye ni mazazi mwenzake na dansa, Moses Iyobo alipata mtoto wa kwanza, Cookie.

Tofauti na Cookie, jina la baba wa mtoto wa pili wa Aunty bado limebaki fumbo kubwa kwani mara zote staa huyo amekuwa akikwepa kumtaja, huku kukiwa na tetesi kwamba huenda baba akawa ni mwanamuziki na mwandishi wa nyimbo za muziki wa  kizazi kipya nchini, Kusah.

Septemba, 2020 wakati Aunty akizundua “Reality Show” yake inayofahamika kwa jina la “Mama Kijacho” ambayo ilikuwa inahusu maisha yake ya ujauzito, mwandishi wa Mwananchi Digital alimuuliza kuhusu baba wa mtoto huyo, lakini Aunty aligoma kujibu.

“Siwezi kusema hapa, maswali yote yanayohusu ujauzito wangu yana majibu yake kwenye reality show yangu. Ukitazama utapata jibu.” Alisema.

Hata hivyo, kwa kipindi chote cha shoo hiyo haikuwahi kuwekwa wazi kuwa ni nani baba wa mtoto.