Balozi EU aipongeza AKU ubora wa elimu

Balozi Manfredo Fanti akihutubia katika mahafali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) jana jijini Dar es Salaam

Muktasari:

  • Takribani wanafunzi 400 wamehitimu katika vyuo vya Aga khan vilivyopo katika nchi za Afrika Mashariki, ambapo  198 kutoka Kenya, 136 kutoka Uganda na 65 kutoka Tanzania.

Dar es Salaam. Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Manfredo Fanti amekipongeza Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kwa kutoa elimu bora ya uongozi katika fani mbalimbali.

Balozi Fanti aliyasema hayo jana Machi 18, wakati alipokuwa anazungumza na wahitimu mbalimbali wa chuo cha Aga Khan nchini Tanzania, ikiwa ni mahafali ya pili baada ya Uviko-19 jijini hapa.

“Siku zote tunahitaji kuwa bora daima na kuongoza kwa mfano kwani hii ndio njia pekee ya kuaminika na Aga Khan wanalifanya hilo kwa kuwaanda wataalamu ambao watakua viongozi bora katika sekta zao,” amesema.

Ameongeza kuwa Tanzania ni nchi inayoendelea kwa haraka na sio tu kiuchumi pia kijamii na kiutamaduni, hivyo ndio maana ni muhimu kuwa na watu ambao ni wataalamu wanaoongoza kwa mfano.

"Nchi ya Tanzania itazidi kukua katika nyanja zote za kimaendeleo endapo vyuo kama Aga Khan wataendelea kuandaa wataalamu na viongozi wa baadae ambao watakwenda kuibadilisha jamii," amesema.

Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha Aga Khan nchini Tanzania AKU, Profesa Eunice Pallangyo amesema wanafunzi waliosoma katika chuo hicho popote wanapoenda huwa ni watu wakuleta mabadiliko.

“Wanafunzi wengi waliosoma Aga Khan na wanaoendelea na masomo wamekuwa ni watu wakuleta mabadiliko kutokana na ujuzi waliokuwanao, mfano namna ya kuhudumia wagonjwa,” amesema

Profesa Pallangyo ambaye pia ni mkuu wa shule ya uuguzi na ukunga aliongeza kwa kusema wanafunzi ambao wamesoma katika chuo cha Aga Khan wengi wao wamekuwa na tabia ya kujiamini wakiwa na malengo ya kuleta mabadiliko katika jamii zao.
“Kujiamini huku kuna kuja baada ya kupata mafunzo sahihi katika fani mbalimbali wanazozisomea na semina tofauti tunazoziandaa ambazo zimekuwa na msaada kwao,” amesema

Mohamed Mushi ambaye ni mmoja wa wahitimu aliyesomea fani ya uuguzi na ukunga amewapongeza wahitumu wenzake kwa kuvumilia kipindi chote wakati wa janga la Uviko-19 hadi kuhakikisha wanafanikisha masomo yao.
“Twendeni tukaibadilishe dunia tuwe viongozi kupitia fani zetu, kwa kuwa mafanikio hayapimwi kwa cheo bali maarifa na ujuzi,” amesema.