Balozi Mushy kuzikwa Moshi Jumanne
Balozi Celestine Mushy
Muktasari:
Balozi Celestine Mushy alifariki Desemba 13, 2022 katika ajali iliyotokea eneo la Mkata wilayani Handeni mkoa wa Tanga baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana na lori la mizigo na kuungua moto akiwa ndani.
Dar es Salaam. Mwili wa Balozi wa Tanzania nchini Austria, Celestine Mushy unatarajiwa kuzikwa Jumanne Desemba 20, 2022 nyumbani kwake Moshi mkoani Kilimanjaro.
Balozi Mushy alifariki Desemba 13, 2022 katika ajali iliyotokea eneo la Mkata wilayani Handeni mkoa wa Tanga baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana na lori la mizigo na kuungua moto akiwa ndani.
Akizungumzia na Mwananchi leo Desemba 16, 2022 kuhusu utaratibu wa mazishi, msemaji wa familia, Dk Kenneth Lema amesema Balozi Mushy atazikwa Jumanne ijayo.
Dk Lema amesema kwa sasa mwili umehifadhiwa mochwari wilayani Handeni lakini kesho Desemba 17, 2022 watausafirisha kwenda Moshi kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.
“Kesho mapema tunatarajia kuuhamisha mwili kuelekea Moshi, baada ya hapo maziko yatakuwa Moshi nyumbani kwake, Kibosho Road, Jumanne ijayo.
“Tutahamisha mwili kutoka Handeni kwenda Moshi, tutaendelea kuuhifadhi hadi maziko, Jumanne,” amesema Dk Lema.
Msemaji huyo wa familia amesema wanashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufanya mipango ya mazishi ya mpendwa wao. Amesema marehemu ameacha mke na watoto wawili.
Wakati huohuo, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje iliyotolewa leo, inaeleza kwamba Balozi Mushy atakumbukwa kwa umahiri wake katika masuala ya kidiplomasia.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba wizara kwa kushirikiana na familia wanaendelea na mipango ya mazishi ya marehemu na taratibu zote zitakapokamilika wananchi watajulishwa.
Balozi Mushy aliteuliwa na Rais Samia Suluhu kuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria Januari 2022 na Mei 5, 2022 akawasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Austria, Alexander Van der Bellen.