Barabara ya lami Vunjo Mashariki yaja

Muktasari:

  • Wananchi wamesema, mara kadhaa viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa ahadi ya kuijenga barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 11, lakini mpaka sasa hakuna kilichotekelezwa. Kitu kinachoongeza gharama za usafiri.

Moshi. Wananchi wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa barabara ya Uchira-Kisomachi-kwa Laria kwa kiwango cha lami, ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao, na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa kata hiyo, wamesema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 11, imetolewa ahadi ya kujengwa na viongozi wa Serikali mara kadhaa lakini bado haijatengenezwa, hali ambayo imekuwa ikiwasababishia usumbufu na gharama kubwa za usafiri.

Melkiori Minja, mkazi wa Kijiji cha Mrumeni katika Kata hiyo, amesema barabara hiyo imekuwa na usumbufu mkubwa hususani kipindi cha mvua na kuiomba Serikali kutimiza ahadi yake hatua ambayo itawapunguzia gharama za usafiri wakazi wa maeneo hayo.

"Barabara  ya Uchira hadi kwa Laria imekuwa na usumbufu mkubwa tumelalamika tumechoka, kila mwaka tunaambiwa itajengwa lakini haijengwi, mwaka 2020 pia aliyekuwa Rais John Magufuli wakati wa kampeni alifika Uchira na kuahidi barabara hii itatengenezwa yote kwa kiwango cha lami, lakini mpaka leo hakuna kilichofanyika," amesema Minja.

Deogratius John amesema kwa sasa wanalazimika kutumia usafiri wa pikipiki ambapo nauli ni Sh3,000 hadi Sh4,000 gharama ambazo ni kubwa na wanaamini barabara hiyo ikitengenezwa kutakuwa na usafiri wa magari na hivyo kupunguza gharama hizo.

"Tunaiomba Serikali iliangalie hili kwani kutoka huku kwenda hadi Uchira imekuwa ni gharama kubwa kutokana na kwamba tunalazimika kutumia usafiri wa pikipiki, na hili pia linatupa wakati mgumu, wakati tunapohitaji kusafirisha mazao kutoka uchira kuja huku kijijini au kutoa ndizi na parachihi huku kupeleka mjini kwa ajili ya biashara". 

Naye Atanas Mrema amesema: "Kuna soko hapa madukani lakini linashindwa kufanya vizuri kwa sababu ya barabara, watu wanashindwa kumudu gharama za kusafirisha bidhaa kutoka mjinj hadi huku, tunaiomba serikali iliangalie hili, ili kuboresha uchumi wetu."

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mrumeni Ewald Malyawere amesema kujengwa kwa barabara hiyo kutapunguza gharama za usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi na hata Taifa.

"Barabara hii imekuwa ni changamoto, tayari imejengwa kilometa moja kwa kiwango cha lami, tunaiomba serikali imalizie hizo nyingine zilizobaki ili kuwezesha kuwepo kwa usafiri wa magari na kupunguzia wananchi gharama za usafiri".

Kwa upande wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Mkoa wa Kilimanjaro, Nicholaus Francis amesema barabara hiyo ipo kwenye orodha ya barabara zilizopo kwenye ahadi za viongozi na kwamba wameendelea na jitihada za kuitengeneza ili kutimiza ahadi hiyo.

"Katika barabara hiyo, kilometa 1.4 imejengwa kwa kiwango cha lami, na mwaka wa fedha 2023/2024 imetengewa Sh750milioni ambazo zitajenga kilometa 1.2, kwa kiwango cha lami na Sh 7milioni kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ili kuwezesha sehemu iliyobaki kupitika vizuri wakato wote".

"Usanifu umekamilika kwa barabara nzima na sasa tunachosubiri ni mfumo wa manunuzi kufunguliwa ili tuweze kumpata mkandarasi na matengenezo hayo yafanyike"