Baraza la Kiswahili laita wakalimani wa Kireno, Kispaniola

Wakalimani kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwa kwenye mafunzo ya kupigwa msasa yanayotolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) kwenye ukumbi wa mikutano wa baraza hilo.

Muktasari:

Bakita inatekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa Ubidhaishaji wa Kiswahili uliozinduliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, Julai 7 ukilenga kuanzisha kanzidata ya wakalimani wa lugha Kiswahili.

Dar es Salaam. Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) limeendeleza utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka 10 wa ubidhaishaji lugha ya Kiswahili kwa kutoa mafunzo ya kuwapiga msasa wakalimani wenye sifa lakini wamekosa uzoefu wa kazi hiyo.

 Hata hivyo, baraza hilo limesema miongoni mwa lugha sita rasmi za Umoja wa Afrika (AU) bado kuna uhitaji wa wakalimani wa Kiswahili kwenda Kireno, na Kispaniola.

Akizungumza leo Agosti 15 kwenye Ukumbi wa Ukalimali uliopo kwenye ofisi ya baraza hilo, Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema serikali kupitia baraza hilo imeanza kuwanoa wakalimani wa Kiswahili kwenda lugha mbalimbali ikiwamo Kispaniola, Kireno, Kichina, Kifaransa, Kiingereza.

Mushi amesema baraza hilo limeamua kuwatumia mwalimu mwenye uzoefu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambaye amebobea kwenye lugha mbalimbali za kigeni ikiwamo Kifaransa.

"Kiswahili sasa ni lugha ya kimataifa na tumeona sasa inatumika katika nyanja mbalimbali hata vyombo vya kikanda na Umoja wa Mataifa vinakitumia," amesema Mushi ambaye ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili.

Amesema baraza limeweka mpango huo wa kuwanoa wakalimani kwa sababu wengi wao wamepata mafunzo ya ukalimani kwa nadharia.

Amesema ili kutatua changamoto hiyo, Serikali iliamua kununua vifaa vya ukalimani ili kuwawezesha kuwaandaa wakalimani kuingia kwenye ushindani katika maeneo mbalimbali wanakoenda kufanya kazi.

Kwa upande wake Katibu huyo Mtendaji amesisitiza kuwa ni muhimu wakalimani wazoefu kuwashika mkono wenzao wanaopatiwa mafunzo ili waweze kuwa na uzoefu pia ni vyema wapewe nafasi katika shughuli ambazo wanazifanya.

"Wapo baadhi ya wakalimani kutokana na kutokuwa na uzoefu wa matumizi ya vifaa vya ukalimani wanajikuta wanashindwa hata kuwasha na kuvitumia vifaa jambo ambalo serikali imelipatia ufumbuzi," amesema Mushi.

Amesema kutokana na ushindani uliopo kimataifa, baraza litahakikisha linawanoa wakalimani wa lugha mbalimbali ili kuwa na watu wanaoweza kufanya kazi katika vyombo vya kikanda na kimataifa.

"Serikali inapowapa fursa kama hii, ni matarajio mtakapohitajika kutoa huduma katika maeneo mbalimbali, ninyi ndiyo mtatumika kwa kazi hiyo," alisisitiza Mushi.

Kwa upande wake mwalimu wa ukalimani, kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Petro Basil  amesema tangu aanze kutoa mafunzo ya msasa takribani wakalimani 600 wameshahitimu mafunzo hayo.

Amesema kwa kuwa wanafunzi hao wa ukalimani wameshaonyesha nia wataendelea kuwanoa huku wakitakiwa kujiamini kuwa wao ni wakalimani.

Naye Mkuu wa Idara ya Ukalimani, wa Bakita, Vida Mutasa amesema mafunzo hayo ni endelevu baraza litaendelea kuwanoa wakalimani kila wakati kulingana na mahitaji.