Barua ya likizo ya Mchungaji Kimaro wa KKKT Kijitonyama yaibua vilio, mjadala

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama Eliona Kimaro.

Muktasari:

  • Usiku wa Januari 16, 2023 ilisambaa video ikimuonyesha mchungaji Eliona Kimaro akiwaeleza waumini wake kuwa amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa katika ofisi ya msaidizi wa askofu na kufanya kikao na mkuu wa jimbo.

Dar es Salaam. Vilio na mjadala vimeibuka mara baada ya kusambaa kwa video ikimuonyesha Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama Eliona Kimaro akiwaaga waumini wake akieleza kuwa amepewa likizo ya siku 60 na uongozi.

Usiku wa jana, Januari 16, 2023 video ikimuonyesha mchungaji huyo akiwaeleza waumini wake kuwa amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa katika ofisi ya msaidizi wa askofu na kufanya kikao na mkuu wa jimbo, ilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

"Semina yetu ni ya wiki mbili (Semina ya neno la Mungu), lakini leo niliitwa ofisi ya msaidizi wa askofu, tulikuwa na kikao na Mkuu wa Jimbo la Kaskazini Mchungaji Mwangomola. Nimepewa barua ya likizo ya siku 60 kesho asubuhi atahubiri Mchungaji Anna na ataendelea kuwa Mchungaji wenu,"

“Kwa mujibu wa barua nitarudi Machi 17 (2023) na sitakuja hapa barua inanilekeza kuripoti Makao Makuu ya Dayosisi kwa hiyo mimi ni mchungaji wa Lutheran kwa hiyo nina heshimu kiapo changu cha kichungaji na kuishi katika kiapo na maadili…

“Pia kwa neema ya Mungu kwa sababu hiyo imenilazimu kutii na kwenda kwenye hiyo likizo na baadaye kuripoti kwenye ofisi ya askofu kama nilivyoelekezwa,” anasema Mchungaji Kimaro katika video hiyo.

Mbali ya video hiyo, ipo nyingine iliyosambaa ikiwaonyesha baadhi ya waumini wa usharika huo wakiangua vilio, wakati mchungaji huyo akifanya maombi ndani ya kanisa hilo wakati akiaga.

Baadhi ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kijitonyama wakiwa na mabango nje ya kanisa hilo leo Januari 17, 2023.

Mwananchi imefika kanisani hapo na kuwakuta baadhi ya waumini ambao wameeleza kuwa baadaye jioni watakuwa na jambo lao, ambalo walidokeza kuwa ni kutaka arudi kazini.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa waumini katika usharika huo, Friday John's ambaye ni muumini wa kanisa hilo amesema… “hatujajua watu watapokeaje hili. Mafundisho yake yametutoa mbali, watu wengi wamekuwa wakifuatilia na kupokea mafundisho yake.

“Tunataka mchungaji wetu arudi mafundisho yake yametusaidia ukiacha uchungaji amekuwa na roho ya kipekee ya kusaidia watu.”

Muumini mwingine, Enea Mwantika amesema mchungaji huyo ndio kwanza alikuwa ameanza semina ya wiki mbili na kwamba barua hiyo ya likizo imewaumiza.

“Kilio chetu kwa Dayosisi tunamtaka Mchungaji Kimaro arudi Kijitonyama kuna mtu amehusika. Sisi ndio tunayemfahamu mafundisho yake wapi yanatupeleka na ni nini tunachokipata,” amesema Mwantika.

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu wa KKKT, Robert Kitundu alisema lipo chini ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

“Kanisa la Kiinjili la Kilutheri lina dayosisi nyingi. Kunapokuwa na dayosisi maana yake kunakuwa na Askofu ambaye anamiliki lile eneo. Mimi kama katibu mkuu wa Kanisa labda nimeambiwe au vinginevyo kwa sasa wazungumzaji ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ambaye ni (Alex) Malasusa au Katibu wake,” alisema.

Mwananchi lilifika katika ofisi kuu za jimbo hilo, Azania Front ambako lilielezwa kuwa Askofu Malasusa yupo nje ya nchi kikazi.

Katibu wa dayosisi hiyo, Goodluck Nkini pia alikataa kuzungumzia suala hilo akieleza kuwa hayo ni mambo ya kichungaji taaluma ambayo alisema hana.

Mwananchi lilimtafuta msaidizi wa Askofu Chediel Lwiza ambaye anaidaiwa kuwa ndiye aliyefanya kikao na Mchungaji Kimaro na mara baada ya mwandishi wa Mwananchi kujitambulisha, alikata simu.

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu utaratibu wa kuhamishwa kwa wachungaji katika Kanisa hilo, Askofu mmoja wa KKKT ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe amesema, “Kila dayosisi ina utaratibu wake. Hapo Dar es Salaam nasikia hata wakuu wa majimbo wanahamishwa.”