Bashe ataka NFRA kutafuta masoko mapya

Bashe ataka NFRA kutafuta masoko mapya

Muktasari:

  • Tanzania ni miongoni mwa mataifa Afrika yanayozalisha mazao cha chakula kwa wingi na kuuza kwenye nchi mbalimbali zikiwemo za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Dodoma. Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ameitaka Bodi ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuchangia kuchochea ukuaji wa uchumi hususani kwa kutafuta masoko ya nje ya nchi.

Pia, Bashe ameishauri NFRA kukodisha baadhi ya maghala yake kwa sekta binafsi ili kujipatia fedha badala ya kuyaacha wazi kama ilivyo kwa sasa.

Ameyasema hayo leo Alhamisi ya Mei 13, 2021 baada ya kumalizika kwa kikao kazi cha bodi hiyo jijini hapa huku akisema wao ni mabawa ya kibiashara kwa Serikali hivyo, hawapaswi kutetereka.

“Najua kuna baadhi ya maghala kwa sasa ni matupu. Badala ya kukaa hivi, bora mngetafuta taasisi au watu waweze kuyakodi na hapa mtapata fedha ya kusaidia shughuli zingine,” amesema Bashe.

Kuhusu masoko, amesema kwa sasa kuna masoko ya chakula kwenye nchi za Sudan Kusini, DR Congo na Kenya, hivyo akawataka kuanza jitihada za kutafuta masoko mapya kupitia mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania kwenye mataifa hayo.

Kwa mujibu wa Bashe, wakala huo wa chakula unatakiwa kuanzisha mawakala zaidi kwa ajili ya masoko ili kuzalisha mapya.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NFRA, Eustance Kangole, amesema wamepokea ushauri huo wa Bashe na kwamba, watakwenda kuufanyia kazi kwa haraka ili kuongeza tija.