Bashungwa atoa kauli sakata la mkurugenzi Temeke kuwaweka chini ya ulinzi wanahabari

Bashungwa atoa kauli sakata la mkurugenzi Temeke kuwaweka chini ya ulinzi wanahabari

Muktasari:

  • Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema inafuatilia malalamiko ya wadau wa tasnia ya habari juu ya mkurugenzi wa manispaa ya Temeke,  Lusabilo Mwakabibi.

Dar es Salaam. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema inafuatilia malalamiko ya wadau wa tasnia ya habari juu ya mkurugenzi wa manispaa ya Temeke,  Lusabilo Mwakabibi.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Mwakabibi kudaiwa kutoa amri ya kuwekwa chini ya ulinzi kwa waandishi wa habari Christopher James wa ITV na Redio One na Dickson Billikwija wa Island TV.

Leo Jumanne Aprili 13, 2021 Bashungwa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, amewataka wanahabari kuwa na subira wakati taarifa hizo zinafanyiwa kazi.

Aprili 12, 2021 waandishi hao inadaiwa kuwa waliwekwa chini ya ulinzi katika kikao kati ya mkurugenzi huyo na wafanyabiashara wa soko la Mbagala rangi tatu.

Inadaiwa kuwa aliwaamuru askari kuwaweka chini ya ulinzi wanahabari hao  mpaka watakapomaliza kikao kwa hatua zaidi.