Bashungwa 'awatega' mameneja Tarura

Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa

Muktasari:

Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amemauagiza katibu mkuu wa Wizara hiyo kumpa taarifa za utendaji kazi wa mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) wa mikoa nchi nzima kila mwezi.

Musoma. Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amemauagiza katibu mkuu wa Wizara hiyo kumpa taarifa za utendaji kazi wa mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) wa mikoa nchi nzima kila mwezi.

Bashungwa amesema kubaki kwenye nafasi hizo kwa mameneja wa mikoa kutategemea na taarifa ya utendaji kazi kwa kila mwezi.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Februari 6, 2022 katika kijinji cha Mugango wilayani Musoma mkoani Mara wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari.

Amesema kuwa taarifa hizo za kila mwezi zinalenga kuleta ufanisi ndani ya wakala huo ili kuwepo kwa thamani ya fedha katika miradi inayotekelezwa.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha utendaji kazi ndani ya wakala huo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ili miradi ya barabara hasa ya vijijini uweze kutekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa.

"Kukaa kwenye nafasi ya meneja wa mkoa kutategemea na taarifa ya utendaji kazi wa meneja husika ya kila mwezi na tunafanya hivi kwasababu tunataka kuona ufanisi tayari nimemuagiza katibu mkuu kusimamia hili na kinachofuata ni utekelezaji tu" amesema Bashungwa

Amesema kuwa kuongezeka kwa bajeti na maboresho ndani ya Tarura kunalenga kuondoa changamoto ya barabara za vijijini ambayo imekuwa ikiwakabili wananchi kwa muda mrefu.

"Mkoa wa Mara pekee umetengewa bajeti ya Sh25.44 kwa mwaka wa fedha 2021/22 kutoka bajeti ya Sh9.7 bilioni ya mwaka 2020/22 na hadi sasa mkoa umekwishapokea Sh11.83 bilioni za bajeti hii kwaajili ya kutekeleza shughuli za Tarura hivyo sisi kama wizara tunataka ufanisi tu na si vinginevyo" amesema.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi alisema mkoa huo umepokea zaidi ya Sh126 bilioni kwaajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuboresha huduma za jamii tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.

"Serikali ya awamu ya sita kwakweli imetutendea haki tangu ilipoingia madarakani changamoto nyingi zinatatuliwa miradi ya maji huko vijijini inaendelea kwa kasi" amesema Hapi

Amesema kuwa fedha hizo zimeweza kutekeleza miradi kadhaa ya maji iliyokwama kwa muda mrefu ambapo ametaja baadhi ya miradi kuwa ni pamoja na mradi wa maji Shirati wilayani Rorya na mradi wa chujio la bwawa la Manchira wilayani Serengeti.

"Maji sasa hivi yanatoka Shirati, Mugumu Serengeti pia wana maji safi na salama, mitaa saba ya manispaa ya Musoma ambayo haikuwa na maji pia muda sio mrefu itapata maji na hii ni kutokana kiasi hicho cha fedha ambacho mkoa wetu umepokea kwa muda huo mfupi " amesema Hapi

Amesema kuwa miongini mwa fedha hizo ni pamoja na Sh4.5 bilioni za Uviko 19 ambazo zimepelekwa mkoani humo kwaajili ya kutekeleza miradi ya maji ambapo amesema kuwa fedha hizo zitagawanywa kwenye majimbo yote 10 ya uchaguzi yaliyopo mkoani humo.