Bavicha wajadili kujaza nafasi ya Nusrat Hanje

Muktasari:

  • Nusrat Hanje ni miongoni mwa wabunge 19 wa viti maalum waliofukuzwa Chadema kwa kosa la kuapishwa kushika nafasi hizo bila ruhusu ya chama hicho Novemba 2020. 

Dar es Salaam. Kamati ya utendaji ya Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) imekutana mkoani Shinyanga, ambapo pamoja na mengine litajadili namna ya kujaza nafasi ya katibu mkuu wa baraza hilo iliyoachwa wazi na Nusrati Hanje aliyefukuzwa uanachama.

Hanje ni miongoni mwa wabunge 19 wa viti maalum waliofukuzwa Chadema kwa kosa la kuapishwa kushika nafasi hizo bila ruhusu ya chama hicho Novemba 2020. 

Hivi karibuni wabunge hao wakiongozwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake, (Bawacha) Halima Mdee, walifungua kesi mahakamani wakipinga kufukuzwa kwao.

Ni baada ya Baraza Kuu la Chadema lililoketi Mei 11, 2022 kuridhia uamuzi wa kamati kuu kuwafukuza.

Tarifa iliyotolewa leo Agosti 11 na mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Bavicha, Apolinary Boniface, imesema kabla ya kujadili suala hilo, kamati hiyo imepata mafunzo kutoka kwa Katibu Mkuu, John Mnyika akisaidiana na Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.

“Asubuhi ya leo Julai 11, 2022 wajumbe wa kamati ya utendaji Bavicha taifa wameshiriki mafunzo ya kiuongozi.

“Kesho pia viongozi hao watashiriki maadhimisho ya siku ya vijana duniani hapa Shinyanga,” amesema.

Kuhusu kuziba nafasi ya Katibu mkuu wa Bavicha, amesema nafasi hiyo hupatikana kwa kuwapigia kura wagombea.