Bawacha wazuiwa kupanda miti Kiboriloni
Katibu Mkuu wa Baraza la wanawake Chadema Taifa (BAWACHA),Catherine Ruge akizungumza na mara baada ya kuzuiliwa kupanda miche ya matunda katika shule ya Sekondari Kiboriloni, iliyopo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Moshi. Viongozi wa Baraza la Wanawake Chadema wamezuiliwa kupanda miche ya matunda katika shule ya Sekondari Kiboriloni, iliyopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, baada ya mmoja wa walimu wa shule hiyo kusema wao sio chama tawala.
Hali hiyo imejitokeza leo Machi 3 wakati viongozi hao wakiendesha kampeni ya kuotesha miti ya matunda na vivuli katika maeneo mbalimbali mkoani humo kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 8.
Akizungumza mara baada ya kutokea sintofahamu hiyo, Katibu Mkuu Baraza la Wanawake wa Chadema Taifa, Catherine Ruge amelaani vikali kitendo hicho na kusema suala la mazingira sio suala la kisiasa.
"Bawacha tulichagua Mkoa wa Kilimanjaro kuja kuadhimisha wiki ya mwanamke kuanzia Machi 3 mpaka Machi 8 ambapo ndio kilele cha maadhimisho haya.
"Katika siku hizo sita tulipanga programu ikiwa pamoja na kupanda miti na tumepanda miti katika zahanati ya Merybennet, Shule ya New St Anne na hapa Kiboriloni lakini kwa masikitiko makubwa tumezuiliwa," amesema.
Amesema baada ya kufika shuleni hapo walimkuta Makamu mkuu wa shule hiyo, akasema hana taarifa na ujio wao na kwamba hawezi kuwaruhusu kufanya shughuli hiyo ya upandaji wa miche ya matunda shuleni hapo.
"Kiongozi wetu wa hapa ambaye ni Diwani anayetokana na Chadema alipeleka barua kwa Mkurugenzi kuhusu hii taarifa na alisema haina shida kwa kuwa suala la mazingira ni suala la maendeleo, lakini kwa masikitiko makubwa tumekutana na changamoto hii," amesema.
Naye Diwani wa kata ya Kiboriloni, Frank Kagoma amesema alifanya mawasiliano na uongozi wa Manispaa juu ya ujio huo wa Bawacha katika shule hiyo na kwamba barua ya mapokezi ya viongozi hao ilisainiwa na makamu Mkurugenzi wa Manaispaa hiyo.
"Tulionge na Kaimu Mkurugenzi akatuambia nendeni shuleni mimi nitafanya mawasiliano nao ili kuhakikisha hili jambo linafanikiwa lakini kwa masikitiko makubwa, mwalimu tuliyemkuta ametupa majibu ambayo sio sahihi," amesema.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Zebedayo Tluay hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari walipomuuliza sababu ya kuwazuia Bawacha na muda alikuwa akizungumza na simu.