Bawacha yapigilia msumari sakata la Pauline Gekul

Mwenyekiti Baraza la Wanawake Chadema Wilaya ya Ilala (Bawacha), Joyce Mwambapa akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 30, 2023 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) limetoa tamko la kulaani tuhuma za unyanyasaji zinazomkabili aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul ambaye pia ni Mbunge wa Babati mjini.

Dar es Salaam. Ikiwa ni takriban wiki moja tangu ziibuke tuhuma za unyanyasaji wa kijana kijana Hashim Ally zinazodaiwa kufanywa na Mbunge wa Babati mjini, Pauline Gekul, Baraza la Wanawake Chadema, (Bawacha) limeibuka na kulaani kitendo hicho likitaka hatua zichukuliwe dhidi mbunge huyo.

Bawacha imeeleza  kusikitishwa na tuhuma hizo dhidi ya mbunge huyo ambaye anadaiwa kutoa maelekezo kwa vijana kumpiga na kumuingizia chupa sehemu ya haja kubwa kijana huyo.

Baraza hilo limesema limeumizwa zaidi kwa kuwa mtuhumiwa alikuwa na dhamana ya kusimamia sheria nchini akiwa naibu waziri wa Katiba na Sheria, wadhifa ambao ulitenguliwa kipindi ambacho tuhuma hizo zimeanza kusamba.

Tamko la Bawacha limekuja katika kipindi cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani, zilizoanza Novemba 25 hadi Desemba 10.

Akiwasilisha tamko hilo mbele ya waandishi wa habari na wajumbe wa baraza hilo leo Alhamsi Novemba 30, 2023, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Ilala, Joyce Mwambapa amesema kitendo cha Gekul kutuhumiwa tu kwa unyanyasaji “ni aibu kubwa’.

"Aibu kubwa si kwake tu bali kwa wanawake wote na wapenda haki na utawala wa sheria na kimsingi hastahili kuitwa kiongozi. Kitendo hicho hakiendani na umama wake. Mama anapaswa kulinda watoto wake," amedai.

Mwambapa amesema kama alivyokuwa angali naibu waziri wa Katiba na Sheria, wanaamini anafahamu utaratibu wa kushughulikia makosa au tuhuma na angekuwa wa kwanza kupinga ukatili wa aina yoyote ile na si kuwa sehemu ya ukatili.

"Bawacha imesikitishwa na tuhuma hizi kwa kuwa hili ni baraza la wanawake ambalo lengo lake ni kutetea wanawake na watoto na kupinga aina zote za ukatili. Tuhuma hizi zimetugusa sana kama wazazi wanawake tuliopitia uchungu wa kuzaa," amesisitiza.

Aidha, Bawacha imeipongeza mamlaka ya uteuzi kwa kutengua uwaziri wa Gekul ili haki iweze kutendeka, hivyo imeomba mamlaka hiyo isiishie hapo, bali iendelee kuchunguza tuhuma nyingine za ukatili wa kijinsia zinazofanywa na viongozi wa Serikali na taasisi zake mbalimbali.

"Pia tunatoa wito kwa Watanzania wote kutoa taarifa za udhalilishaji na ukatili wa kijinsia. Hili ni jukumu letu wote kushiriki kwenye mapambano dhidi ya ukatili huo.

“Mwisho, tunaitaka Serikali kupitia vyombo vyake kusimamia jambo hili bila upendeleo na kwa uwazi huku tukiomba ulinzi kwa vijana hao ili ushahidi usipotee," amemalizia Mwambapa.

Tuhuma za Gekul pia zimezungumzia na Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mkoa na Taifa, kikiahidi kucachukua mkondo wake kwa kuwa kina kanuni na taratibu na kuvitaka vyombo vya dola kulishughulikia.

Mbali na CCM, pia Jumuiya yake ya wanawake (UWT) ilijitokeza na kulaani tuhuma hizo na kutaka vyombo vya dola kufanya haraka uchunguzi na akibainika kuhusika hatua kali zichukuliwe dhidi yake.

Kadhalika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB) imesema inachunguza sakata hilo ili kupata ukweli wa tuhuma hizo.

Tayari Gekul ambaye hajajitokeza hadharani kuzungunzia sakata hilo, amehojiwa na Polisi mkoani Manyara na kuachiwa.