BBI inavyoongeza fukuto la uchaguzi mkuu Kenya

BBI inavyoongeza fukuto la uchaguzi mkuu Kenya

Muktasari:

  • Mbio za uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika mwaka 2022 zimezidi kupamba moto nchini humo, wakati Rais Uhuru Kenyatta akijaribu kufanya mabadiliko ya mfumo wa uongozi ambao utaondoa ghasia za baada ya uchaguzi.

Mbio za uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika mwaka 2022 zimezidi kupamba moto nchini humo, wakati Rais Uhuru Kenyatta akijaribu kufanya mabadiliko ya mfumo wa uongozi ambao utaondoa ghasia za baada ya uchaguzi.

Rais Kenyatta pamoja na kiongozi wa upinzani, Rais Odinga wamekubaliana kuwaunganisha Wakenya na kuifanya nchi hiyo iwe na amani wakati wote na chaguzi zisiwe chanzo cha vifo kwa wananchi wa Kenya.

Viongozi hao wameanzisha Mpango wa Kujenga Madaraja (BBI) ambao unalenga kuleta amani, kujenga umoja wa kitaifa na kuondoa ghasia za baada ya uchaguzi kama ilivyozoeleka kila unapofika msimu wa uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge.

Hata hivyo, Naibu Rais wa Kenya, William Ruto ambaye ameonyesha nia ya kuwania urais mwaka 2022, anapinga mpango huo kwa madai kwamba huu si wakati wa kujadili namna ya kugawana vyeo, bali kujadili namna watu masikini watakavyoendesha maisha yao.

Rais Kenyatta na Odinga wamekuwa wakitembea sehemu mbalimbali za nchi hiyo wakiipigia chapuo BBI, wakati Ruto pamoja na wafuasi wake wanaojiita “hustlers” (wapambanaji) nao wakizunguka kueleza kwanini wanaipinga BBI.

Wanasiasa wa Kenya wamekuwa wakiitumia BBI kufanya kampeni za wazi wakati wakijiandaa na uchaguzi mkuu wa mwakani ambapo mpaka sasa wanaotajwa kuwania urais ni pamoja na Ruto na Odinga.

Chanzo cha BBI

Kenya ni nchi ambayo ilikumbwa na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2013 ambapo watu zaidi ya 1,000 walipoteza maisha yao kutokana na uhasama wa kisiasa baina ya pande mbili za kisiasa zilizoshiriki uchaguzi huo.

Rais Kenyatta alifanikiwa kushinda uchaguzi huo na mgombea mwenza wake, Ruto akawa Naibu Rais wa Kenya. Itakumbukwa kwamba baada ya uchaguzi huo viongozi hao walianza kuitekeleza Katiba mpya iliyokuwa imeandikwa.

Kiongozi wa upinzani na mgombea urais katika uchaguzi huo, Odinga hakukubali matokeo kwa madai kwamba uchaguzi ulitawaliwa na udanganyifu mkubwa na alivilaumu vyombo vya dola kuua watu waliokuwa wakipinga matokeo hayo.

Rais Kenyatta na Ruto walishitakiwa katika Mahakama ya Uhalifu ya The Hague iliyopo huko Uholanzi. Hata hivyo, mashitaka dhidi yao yalitupiliwa mbali na Mahakama hiyo kwa sababu ya kukosekana ushahidi wa kutosha.

Siasa ziliendelea, Rais Kenyatta akatawala kwa miaka mitano, ukafika wakati wa uchaguzi mkuu mwingine mwaka 2017. Rais Kenyatta aligombea kwa muhula wake wa pili huku akishindana na mpinzani wake, Odinga.

Uchaguzi ulikuwa na ushindani mkubwa, hata hivyo, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) ilimtangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi katika uchaguzi huo, wapinzani hawakuridhika, wakafungua shauri mahakamani kupinga matokeo hayo.

Kwa mara ya kwanza Mahakama ya Kenya kupitia kwa Jaji Mkuu, David Maraga pamoja na majaji wengine watano walibatilisha matokeo ya uchaguzi wa Agosti 2017 yaliyompa ushindi Rais Kenyatta.

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Juu, uchaguzi ulirudiwa na Rais Kenyatta alishinda kwa asilimia 98 baada ya wapinzani kususia uchaguzi huo ambao asilimia 39 ya wapigakura pekee ndiyo walijitokeza.

Novemba 28, 2017, Kenyatta aliapishwa kuwa Rais wa Kenya kwa muhula wake wa pili, jambo ambalo wapinzani hawakulikubali. Januari 30, 2018, Odinga alijiapishwa kama Rais wa Watu wa Kenya.

Kutokana na mgawanyiko wa Wakenya, Rais Kenyatta alifanya mazungumzo na mpinzani wake, Odinga na kwa pamoja walikubaliana kuwaunganisha Wakenya kwa ishara ya kupeana mkono maarufu nchini humo kama “Handshake.”

Rais Kenyatta na Odinga waliunda kamati ya BBI ambayo ilizunguka kukusanya maoni ya wananchi na kutoa ripoti ambayo ilitoa mapendekezo mbalimbali, ikiwamo kuundwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu, mawaziri kuteuliwa kutoka bungeni tofauti na sasa.

Kamati ya BBI iliangazia masuala tisa, ikiwamo ukabila, ufisadi na ugatuzi, miongoni mwa changamoto kuu ambazo zimelikabili Taifa hilo tangu lilipopata uhuru wake mwaka 1963.

Ajenda nyingine zilikuwa ni pamoja na jinsi ya kumaliza migawanyiko ya kikabila, kuwashirikisha watu wote kuhusu masuala ya utawala na siasa za Kenya, jinsi ya kushughulikia suala la kumaliza uhasama wa kisiasa unaotokea wakati wa uchaguzi mkuu,

Vilevile ilizingatia namna ya kuimarisha amani na usalama, kukabiliana na janga la ufisadi, kukabiliana na ukosefu wa maadili ya kitaifa, masuala ya majukumu na haki za raia, kuwajibika kwa pamoja na jinsi ya kuendeleza serikali za ugatuzi.

Joto la uchaguzi lapanda

Wakati Rais Kenyatta akikaribia kumaliza muda wake madarakani, amekuwa na mvutano wa dhahiri na Ruto kutokana na tofauti yao ya kimtazamo kuhusu BBI ambayo iliasisiwa na Rais Kenyatta pamoja na mpinzani mkuu, Odinga.

Rais Kenyatta amekuwa akituhumiwa kutaka kujiongezea muda wa kukaa madarakani, hata hivyo, amekuwa akisisitiza kwamba hana mpango wa kubadilisha Katiba ili ajiongezee muda, bali yeye na Odinga wanataka kuijenga Kenya moja yenye amani wakati wote.

Hata hivyo, Ruto anaiona BBI kama mpango wa Rais Kenyatta kumzuia kuwa Rais wa Kenya mwaka 2022 kama ambavyo walikubaliana wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2013 ambapo walipata ushindi.

Ruto amekuwa akizungumzia mambo mbalimbali mazuri ya kijamii ambayo serikali imefanya, lakini akipingana na BBI kwa madai kwamba huu siyo wakati wa kujadili namna ya kugawana madaraka, bali kuwawezesha watu masikini kama mama mboga wanaoishi maisha magumu.

Wananchi wa Kenya ndio waamuzi wa mwisho katika kuipitisha BBI kupitia kura ya maoni ambayo itatoa nafasi ya mabadiliko ya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010 ili kuruhusu mfumo mpya wa utawala.

Bado haijafahamika ni lini kura ya maoni itaitishwa, hata hivyo, IEBC imesema itahitaji Sh15 bilioni (za Kenya) ili kuendesha kura hiyo ya maoni. Watu wengi wanaona bora fedha hizo zielekezwe kwa Wakenya ambao shughuli zao za kiuchumi zimeathiriwa na janga la corona.

Wanasiasa wa Kenya wamegawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza ni lile linaloitetea BBI likiongozwa na Rais Kenyatta na Odinga; na la pili ni lile linaloipinga BBI likiongozwa na Ruto pamoja na baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakiikosoa serikali.

Februari 15, Rais Kenyatta alimtaka naibu wake, Ruto ajiuzulu kwa sababu amekuwa akikosoa miradi ya serikali wakati yeye pia yumo ndani ya hiyo serikali. Alisisitiza kuwa serikali ni moja, kama kuna mazuri ni ya serikali na kama anaona kuna mabaya ajiondoe serikalini ili akaikosoe.