Bei mafuta yazidi kutesa madereva

Bei mafuta yazidi kutesa madereva

Muktasari:

  • Bei ya petroli imeendelea kuongezeka na kufikia kiwango cha juu zaidi ndani ya miezi 32 iliyopita, hali inayowapa ugumu madereva wakiwamo wa daladala, Mwananchi limebaini.

Dar es Salaam. Bei ya petroli imeendelea kuongezeka na kufikia kiwango cha juu zaidi ndani ya miezi 32 iliyopita, hali inayowapa ugumu madereva wakiwamo wa daladala, Mwananchi limebaini.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza kupanda kwa bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kuanzia Agosti 4 mwaka huu.

Bei ya petroli iliyotangazwa kuanzia juzi ni Sh2,427 ikiwa ni kubwa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili ukilinganisha na Sh2,436 ya Disemba 2018.

Bei hizi mpya pia zinamaanisha kuongezeka kwa asilimia 60 kwa bei ya petroli Tangu Juni 2020 bei ilipotangazwa kuwa Sh1,520. Hili ni ongezeko la Sh907.

Katika kipidi hicho bei ya dizeli ilipanda kwa asilimia 46 hadi Sh2,251 sawa na ongezeko la Sh705 wakati mafuta ya taa yakipanda kwa asilimia 39 hadi shi 2,176 ikiwa ni Sh608 zaidi.

“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji,” ilitaja ripoti ya Ewura katika vipindi tofauti isipokuwa mwezi Julai ambapo licha ya sababu hizo, kulikuwapo na mabadiliko ya tozo na ada kwenye mafuta yaliyofanywa na Serikali.

Hali ni mbaya kwa madereva wanaolia bei ya mafuta kuendelea kupanda kila mwezi, wakisema wanalazimika kuongeza mizunguko wanayofanya kazi ili waweze kupata posho zao.

Saidi Kipandi, dereva wa daladala za Makumbusho hadi Bunju mkoani Dar es Salaam, alieleza kuwa bei za mafuta zinawaumiza kwa kuwa zimepunguza kiasi cha posho walizokuwa wakilipwa.

“Changamoto tunayoipata kubwa ni pale mabosi wanapohitaji hesabu ileile. Unapotoa pesa ya mafuta unakuta posho yako inabaki Sh5,000” alifafanua Kipandi.

Dereva mwingine Gasper Kunambi alisema yeye anaendesha magari ya shamba (yanayotoka nje ya mji) ambayo hayana wateja, hivyo anapofanya kazi anafikiria kwanza namna ya kufikisha hesabu, fedha ya kulaza gari na mafuta, kisha posho yake ambayo imekua chini sana au asipate kabisa katika baadhi ya siku.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) Mustapha Mwalongo, alisema biashara imekua ngumu sana na wanafanya biashara kwa hasara.

‘‘Sasa tupo kwenye mchakato wa kutoa mapendekezo kwenye mamlaka husika kama wanaweza kubadilisha viwango vya nauli,’’ alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac) Raphael Mgaya alisema bei imeongezeka kwenye soko la dunia na bei iliyopo sasa nchini inaakisi huko yanapotoka.

Akizungumzia athari wanazopata alisema,”... kupanda kwa bei kunafanya uhitaji wa mafuta kupungua, hivyo biashara inakua ngumu na gharama za uendeshaji zinaongezeka pia”. Mwananchi lilipojaribu kuhoji makadirio ya bei katika miezi inayofuata Mgaya alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia hilo.