Bei ya vyakula maumivu

Mfanyabiashara, Jackson Mahuwi (kulia) akimpimia mteja mchele alipokwenda kununua bidhaa hiyo katika Soko la Mwananyamala, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Sunday George

Muktasari:


Wakulima waeleza sababu nyuma ya pazia, Serikali yatoa kauli

Dar/mikoani. Wakati bei za vyakula zikizidi kupanda katika maeneo mbalimbali nchini, wakulima wametaja sababu tatu za hali hiyo, wakiitaka Serikali kuingilia kati.

Miongoni mwa sababu hizo, eneo ambalo wanataka Serikali iingilie kati ni kufurika kwa wanunuzi wa nafaka kutoka nje ya nchi. Sababu nyingine ni mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la bei ya pembejeo.

Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti na wakulima, wafanyabiashara na Serikali walipozungumza na gazeti hili.

Wakati hayo yakielezwa, bei ya mchele na maharage kwa lejaleja katikja maeneo kadhaa imegonga Sh3,000 na ushei huku unga wa mahindi ukiuzwa Sh2,000 na kuendelea katika baadhi ya maeneo.

Mkulima wa mahindi katika Kijiji Cha Isimani, Oscar Ngole alisema ukosefu wa mbolea mwaka jana na ukame uliokuwepo vimesababisha kupanda kwa bei ya mazao mwaka huu.

“Mwaka juzi nililima ekari 10 nikavuna gunia zaidi ya 100, lakini mwaka jana nimelima ekari tatu na nimevuna gunia 20 kwa sababu bei ya mbolea ilikuwa haishikiki, unadhani nitauza bei gani?” alisema Oscar.

Hata hivyo, alisema bei ya mwaka huu inaweza kupanda mara dufu kwa sababu mavuno ni kidogo ikilinganishwa na mwaka jana.

“Ushauri wangu, wakulima wasiuze mazao yote, wabakize chakula vinginevyo hali ya chakula itakuwa mbaya,” alisema.

Yusuph Omary, mkulima kutoka Mbeya anaungana Ngole akisema bei ya sasa imekuwa juu kwa sababu gharama za kilimo zilipanda na kuwaomba wananchi kukubaliana na hali ilivyo.

Katika kushughulikia suala hilo, Serikali ilitangaza mpango wa kutoa ruzuku katika mbolea ili kuweka ahueni kwa wakulima.

Mbali na bei ya pembejeo, mkulima kutoka Nduli, Manispaa ya Iringa, Oliver Mgeni yeye alitaja uhaba wa mvua kwenye maeneo mengi kuwa ndiyo sababu ya bei ya vyakula kupanda.

Hata hivyo, alisema bei wanayouza wakulima ni tofauti na ile inayowekwa na wafanyabiashara masokoni.

“Wafanyabishara wanaongeza gharama za usafiri kwa hiyo bei ya huku si kubwa kiasi hicho,” alisema Mgeni.

Kwa upande wake Ignas Malenga wa Iringa, mkulima wa mpunga alisema wakulima hawajapandisha bei ya vyakula bali hali ya hewa na kupungua kwa maji.

“Gunia la mpunga linaweza kufikia mpaka Sh150,000 tusipokaa vizuri, cha msingi tuombe mvua za mwaka huu ziwahi,” alisema Malenga.

Mkulima wa mahindi wa Songea, Eusebius Wella alisema kupanda kwa bei ya mahindi kumetokana na mahindi kupungua huku kukiwa na mahitaji makubwa baada ya wanunuzi kutoka nje kuyatafuta kwa wingi hadi mashambani kwa wakulima.

Kufuatia hali hiyo, mmoja wa wafanyabiashara katika soko la nafaka Tandale jijini Dar es Salaam, Hemed Hussein alishauri Serikali izuie watu kutoka nje ya nchi kuchukua mchele na mahindi kwa kuwa wanapaisha bei na wao kushindwa kushindana nao sokoni.

“Nchi hizo zina hela ila hawana chakula, hawa ndiyo wanapanga bei wanayotaka. Hali hii inafanya vyakula kupanda bei ndani, mfano kilo moja ya mchele ilikuwa Sh1,800 hadi Sh2,000 kwa ule wa bei ya juu, lakini sasa umefika Sh2,400 hadi Sh2,800 huku gunia tukinunua kati ya Sh130,000 hadi Sh250,000,” alisema.

Madai hayo ya Hussein yanashabihiana na ya Seleman Issa, muuzaji mwingine wa nafaka, aliyesema Serikali inapaswa kutafakari kuhusu suala la kufungua mipaka akihofia kuwa huenda chakula kilichopo hakiwatoshelezi Watanzania.

Akizungumzia hilo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Exhaud Kigahe alisema wameliona suala hilo na wanalifanyia kazi.

Hata hivyo, Kigahe alisema kama nchi, hawaoni kama ni sahihi kupiga marufuku wachuuzi hao kwa kuwa ni jambo litakaloumiza wakulima.

“Wakulima walikuwa na kilio cha kukosa masoko muda mrefu, mazao yalikuwa yakiharibika shambani, tumetafuta masoko ili wafurahie wanachofanya, ila kama Serikali tunataka wafanyabiashara hao wafuate utaratibu,” alisema Kigahe.

“Kama kutakuwa na haja baadaye tutafanya hivyo (kufunga) ila kama Serikali kuna hatua mbalimbali tunazofanya ili kulinda wananchi wetu ikiwemo kuwa na hifadhi ya chakula,” alisema Kigahe.

Alisema wanunuzi wa mazao kutoka nje wanatakiwa kutumia vyama vya ushirika kupata mazao au kununua katika masoko na minada, ila si kwenda nyumbani kwa wakulima.

Alisema kununua mazao nyumbani kumekuwa kukiwafanya wachukue kwa bei ndogo tofauti na iliyopo sokoni, hivyo akasema wizara yake kwa kushirikiana na wizara ya Kilimo na ile ya Tamisemi wamekuwa wakishughulikia suala hilo kila moja kwa nafasi yake.

“Lakini pia ugonjwa wa virusi vya korona na vita ya Ukraine na Russia vimechangia kupandisha bei za bidhaa kwa kiasi na katika kulitambua hilo Serikali imefanya jitihada mbalimbali ili kuleta ahueni kwa wananchi,” alisema Kigahe.

Wakati akisema hayo, vilio vya bei za bidhaa vimezidi kusikika katika maeneo mbalimbali nchini.

Rose Bruno, mwenyekiti mamalishe katika Soko la Kisutu alisema licha ya kupanda kwa mchele, bei ya chakula imebaki kuwa Sh2,000 kwa sahani, jambo ambalo linawaumiza.

“Rais Samia Suluhu atusaidie, hali za mamalishe ni mbaya kibiashara kutokana na hali hii. Hili linawezekana kwani mafuta nayo yalikuwa juu lakini sasa hadi Sh4,000 unapata lita moja,” alisema.

Kadhalika, Asha Ally, mwenyekiti mamalishe soko la Tandale alisema upandaji bei ya mchele umefanya idadi ya wauzaji wa chakula kupungua sokoni hapo kwa kuwa hawaoni faida katika biashara hiyo.

Vilio vya jijini Dar es Salaam havitofautiani na mikoa mingine ambapo wananchi na wafanyabiashara wamepaza sauti zao.

Jijini Dodoma, baadhi ya bidhaa za vyakula bei yake imepaa ukilinganisha na bei za bidhaa hizo kwa kipindi cha miezi kadhaa iliyopita ingawa mafuta ya alizeti yameanza kushuka bei.

Katika maduka na soko la Sabasaba maharage yamepanda kutoka kati ya Sh2,200 na Sh2,300 hadi kati ya Sh2,900 na Sh3,000.

Kwa upande wa unga wa mahindi, Issa Ramadhan mkazi wa Dar es Salaa alisema bei imepanda kutoka kati ya Sh9,000 na Sh12,000 kwa kilo tano hadi kati ya Sh16,000 na Sh17,000 hukubei kuu ya kilo moja ikiuzwa Sh1,800 hadi Sh2,000.

Hali kama hiyo ipo pia mkoani Morogoro ambako ndani ya mwezi mmoja mchele umepanda kutoka Sh1,900 hadi Sh3,000 kwa daraja la kwanza wakati daraja la mwisho ukitoka Sh800 hadi Sh2,400.

Katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, bei ya vyakula na nafaka imeendelea kupanda huku maharage yakiongoza baada ya kufikia Sh3,000 kwa kilo.

Imeandikwa na Aurea Simtowe, Nasra Abdallah (Dar), Mussa Juma (Arusha), Juma Mtanda (Morogoro), Mgongo Kaitira na Saada Amir (Mwanza), Rehema Matowo (Geita), Beldina Nyakeke (Musoma), Rajabu Athumani (Handeni), Stephano Simbeye (Songwe), Hawa Mathias (Mbeya), Mainda Mhando, (Dodoma), Seif Jumanne(Njombe), Bosco Mwinuka(Ludewa) Joyce Joliga (Songea) Tumaini Msowoya (Iringa).