Bei ya zamani ya vifurushi kurejea ‘mdogomdogo’

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mpya wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Dk Jabiri Bakari amesema suala la kurudisha bei za zamani za vifurushi vya mawasiliano litakamilika hivi karibuni na mamlaka hiyo inafuatilia kwa karibu

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mpya wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Dk Jabiri Bakari amesema suala la kurudisha bei za zamani za vifurushi vya mawasiliano litakamilika hivi karibuni na mamlaka hiyo inafuatilia kwa karibu

Suala la vifurushi vya huduma za simu na bei yake lilianza kuumiza vichwa watumiaji wa huduma za simu Aprili 2, 2021 baada ya kuanza kutumika kwa kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalumu zilizotungwa na TCRA.

Tofauti na matarajio ya wengi, baada ya kuanza kutumika kwa kanuni hizo bei za vifurushi ziliongeka, jambo lililoibua kelele miongoni mwa watumiaji kiasi cha TCRA kusitisha matumizi ya gharama mpya.

Baada ya kusitisha, Mkurugenzi Mtendaji wa wakati huo, James Kilaba alisema ingechukua hadi siku 4 vifurushi vya zamani kurejea.

“Maelekezo yaliyotolewa awali yalikuwa na pande mbili, masuala ya bei lakini pia idadi ya vifurushi, suala la kupunguzwa kwa idadi ya vifurushi tayari limefanyiwa kazi vimerudi kama zamani, suala la gharama linaendelea na nina imani halitachukua mwezi mzima, litakamilika mapema,” alisema Dk Bakari.

Dk Bakari aliliambia gazeti hili kuwa kurudisha vifurushi kama zamani linahitaji muda (bila kuutaja) lakini nao wanasimamia kwa karibu kuhakikisha linakamilika na kuna mambo yamekwishabadilika.

“Mwanzo walipewa mwezi mzima kuunda vifurushi vipya, system (mfumo) inahitaji muda, ukiangalia kidogo baadhi ya vifurushi vimebadilika, nasi tunaratibu kwa karibu na tutalitolea mrejesho,” alisema Dk Bakari, ambaye siku ya kuapishwa Rais Samia Suluhu alimsihi kuangalia jambo hilo la vifurushi.

Dk Bakari alisema ambacho kimerudi mpaka sasa kama zamani ni kuondoka kwa ukomo wa idadi ya vifurushi kwa watoa huduma tofauti na kanuni zilivyokuwa zinaelekeza kuwa havitakiwi kuzidi 50.

Katika mitandao ya kijamii watumiaji wa simu bado wanajadili juu ya vifurushi vipya vilivyoanzishwa takribani wiki mbili zilizopita, wengine mara kwa mara wanaziandikia kampuni katika kurasa zao za mitandao ya kijamii wakidai vifurushi vya awali virejeshwe.

Katika mtandao wa Twitter, Vodacom iliwajibu wateja wake waliotoa malalamiko ya kutorudishwa kwa vifurushi kuwa, “tungependa kukufahamisha kuwa mabadiliko yamefanyiwa kazi na tumerudisha bei za vifurushi kama ilivyokuwa awali. Kuna vifurushi tumevisitisha ili kubaki na vifurushi vichache vyenye kutoa huduma bora”.

Kadhalika walimjibu mwingine kuwa “tunaomba ufahamu kuwa kulingana na mwongozo uliotolewa na mamlaka ya usimamizi wa mawasiliano tulibakiwa na vifurushi vichache. Vifurushi vilivyorudi kama zamani baada ya mabadiliko ni intaneti supa, ya kwako tu, supa uni na red relax”.

Mtandao wa Airtel wenyewe uliwajibu wateja kuwa, “kwa sasa kuna mabadiliko ya vifurushi. Tafadhali bofya *149*99#Ok kisha chagua 7 ofa maalumu kisha chagua 4 ili uweze kupata vifurushi kulingana na matumizi yako.”

Na Mtandao wa Tigo ulisema, “tunapenda kukufahamisha kuwa mabadiliko yameanza kufanyika kwa baadhi ya vifurushi vya combo na vya internet, tafadhali tembelea menyu yetu ya *147*00# au *148*00# kwa vifurushi mbalimbali, tutakujulisha pindi kutakapokuwa na mabadiliko ya ofa maalumu”

Mwanzoni mwa Machi, TCRA ilitangaza utekelezaji wa kanuni hizo mpya za kukabiliana na malalamiko juu ya huduma za vifurushi zinazotolewa na kampuni mbalimbali za simu nchini utaanza Aprili 2, 2021.

Kanuni hizo ziliandaliwa kufuatia maoni 3,278 yaliyotolewa na wananchi kuhusu vifurushi hivyo na kumlazimu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, Dk Faustine Ndugulile kuingilia kati.