Benki kuongeza ukopeshaji kukwamua uchumi

Muktasari:

Licha ya ukopeshaji nchini kuathirika na janga la Uviko-19, benki zimeahidi kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kutokana na kuimarika kwa uchumi wa dunia.

Dar es Salaam. Licha ya ukopeshaji nchini kuathirika na janga la Uviko-19, benki zimeahidi kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kutokana na kuimarika kwa uchumi wa dunia.
Pia, hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kwa sasa, zimetajwa kuchochea hali hiyo.
Taasisi hizo za fedha ziliweka bayana mpango huo uliomalizika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma wakati wa Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha (COFI 2021), ambapo wanachama wameahidi kuimarisha ukopeshaji ambao utasaidia uzalishaji na kuukwamua uchumi wa Taifa dhidi ya janga la Uviko-19.
Kwa mujibu wa viongozi waandamizi wa benki hizo, hilo litawezekana kwa kuwa taasisi hizo za kifedha nchini zina uwezo wa kukopesha zaidi na kwa riba rafiki.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema kuwa juhudi za pamoja ni muhimu na ushirikiano wa wadau wote unahitajika.
“Janga la Uviko-19 limekuwa na athari kubwa kwenye benki zetu kuikopesha sekta binafsi,” amesema Zaipuna wakati akizungumza kwenye kongamano hilo alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu kuongeza mikopo kwa sekta binafsi baada ya janga la Uviko-19.
“Ili kuchochea ukopeshwaji wa sekta binafsi baada ya janga la Uviko-19, mambo kadhaa yanabidi kufanywa na wadau husika. Hatua hizi zinahitaji mbinu shirikishi ili kuhakikisha matokeo endelevu ya kiuchumi,” amesema Zaipuna.
Hata hivyo, amesema kuwa tayari kuna mazingira wezeshi ya kuongeza mikopo na ustahimilivu stahiki wa kisekta wa kuchochea kufufua ukopeshaji.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema hali itakuwa nzuri zaidi mwakani kutokana na kupungua kwa athari za Uviko-19 hivyo, uchumi wa Taifa utakuwa kwa asilimi 5.2.
Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha uliofunguliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan uliandaliwa na BoT kwa kushirikiania na Umoja wa Mabenki nchini (TBA) kujadili uimarishaji wa uchumi wa Tanzania kufuatia janga la Uviko-19.
Kabla ya janga la Uviko-19, mikopo kwa ajili ya sekta binafsi ilikuwa inakua vizuri na kifikia asilimia 11.1 mwishoni mwa mwaka 2019, lakini hali ilibalika ghafla baada ya dunia kugubukwa na janga hilo.
Ukuaji huo ulipungua hadi asilimia 5.5 katikati  ya mwaka jana na hali ilizidi kuwa mbaya miezi iliyofuata.
Hata hivyo, Zaipuna amesema kumekuwepo na maendeleo mazuri hivi karibuni kutokana na kuimarika kwa uchumi wa dunia na jitihada za Serikali pamoja na benki kuimarisha na kurahisisha upatikanji wa mikopo.