Benki ya NBC yakabidhi trekta kwa wakulima wa korosho Mtwara

New Content Item (1)
New Content Item (1)

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa zawadi mbalimbali zikiwemo baiskeli, pikipiki na trekta kwa washindi wa  msimu wa  pili wa kampeni ya benki hiyo ya ‘Vuna Zaidi na NBC Shambani’ inayohusisha mkoa wa Mtwara.
Kampeni hiyo inalenga kuchochea kiwango cha uzalishaji wa zao la korosho na mazao mengine katika mkoa huo kwa mujibu wa benki hiyo.

Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa hafla fupi ya kuhitimsha kampeni hiyo sambamba na kukabidhi zawadi kwa washindi wa kampeni hiyo ikiwemo zawadi kubwa ya trekta kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi Mtwara (MAMCU), Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas alisema zawadi hizo zimekuja wakati mwafaka kwa kuwa mkoa huo kwasasa unatekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa korosho kutoka tani 400,000 za sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka 2025

“Ni mpango wa serikali kuona sekta ya kilimo inakua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, hivyo tunashukuru kuona benki ya NBC inashiriki kikamilifu katika kufanikisha azma hiyo kupitia NBC ‘Vuna Zaidi na NBC Shambani’’ alisema Kanali Abbas huku akiwaomba wataalamu wa kilimo mkoani humo kuwatembelea wakulima mara kwa mara ili kuwapa elimu itakayowawezesha kuzalisha korosho bora.

Aidha alisisitiza wakulima wa mkoa huo kuhakikisha wanahifadhi fedha zao benki pamoja na kuwa na nidhamu ya fedha ikiwa ni pamoja na kuwekeza zaidi kwenye ununuzi wa vifaa vya kilimo cha kisasa ili kuongeza uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Waziri Barnabas alisema tangu kuanza kwa kampeni hiyo, jumla ya washindi 73 wakiwemo wakulima mmoja mmoja, vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika kutoka mkoa huo waliibuka washindi na kupata zawadi mbalimbali likiwemo trekta moja, guta (toyo Tri Cycle) mbili, Pikipiki 12, Pumpu za kupulizia dawa miti ya mikorosho 40, Baiskeli 20 vyote vikiwa na jumla ya thamani ya Sh150 milioni kampeni hiyo ya miezi mitatu ilianza Oktoba 13, 2022.

"Bado natoa wito kwa wakulima kuendelea kupitisha fedha zao za malipo ya korosho kupitia akaunti zao za 'NBC Shambani' ili kupata fursa ya kufurahia zaidi manufaa yatokanayo na akaunti hiyo," alisema.

Aidha alisisitiza kuwa benki hiyo imedhamiria kushirikiana vyema na wakulima ili kuhakikisha wanaboresha sekta ya kilimo na kwamba mbali na kampeni hiyo ya ‘Vuna Zaidi na NBC Shambani’ benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo mbalimbali kwa vyama vya msingi mbalimbali katika mikoa hiyo ikiwa ni namna ya kusaidia utendaji kazi wao katika shughuli zinazohusiana na uzalishaji wa korosho.

Kwa upande wao washindi wa droo hiyo waliishukuru NBC kwa kuandaa kampeni hiyo kwani imeonekana kuwa msaada mkubwa kwao huku wakibainisha kuwa siri ya ushindi wao ni kuitumia zaidi benki hiyo katika kupitisha malipo yao yatokanayo na mauzo ya zao la korosho.

"Tunashukuru sana Benki ya NBC kwa zawadi ya trekta hili kwa kuwa itatusaidia sana kufikia malengo yetu. Pia tunaahidi kuendelea kuelekeza fedha zetu kupitia akaunti ya ‘NBC Shambani’ ili kujishindia zawadi nyingi zaidi,’ alisema Siraji Mtenguka, Mwenyekiti wa MAMCU ambaye taasisi yake imejishindia zawadi ya trekta kupitia kampeni hiyo kwa mara ya pili mfululizo