Benki zaja na mfumo bora wa utoaji huduma kwa njia za kidigitali
Muktasari:
- Jinsi maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanavyochagiza kuwapo na mifumo bora ya utoaji wa huduma za kibenki kwa haraka na usalama Zaidi, huku zikiwawezesha wafanyabiashara kupata suluhu mbalimbali za kibenki kwa njia ya Kidigitali.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha kuna mifumo yenye ubora inayoendana na mapinduzi ya Sayansi na Teknolojia, Benki ya Standard chartered yaja na mfumo ambao utaboresha utoaji wa huduma za kibenki kwa haraka na usalama zaidi, na kuwezesha wafanyabiashara kupata suluhu mbali mbali za kibenki kwa njia ya kidijitali.
Akizungumza na Mwananchi mara baada ya uzinduzi wa mfumo huo, leo Mei 17, katika hotel ya Hyatt, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Tanzania, Dk. Nkundwe Moses Mwasaga ambae ndie alikua mgeni rasmi amesema,
"Nimefurahi kuwa shahidi wa uzinduzi wa mfumo wa ‘Straight2Bank Next Gen’ ambao utaboresha huduma na kutatua changamoto za benki kwa wateja hasa wafanyabiashara nchini Tanzania,”
Ameongeza kwa kusema wanaendelea kukubali mageuzi ya mifumo ya kidigitali katika uchumi wetu, kwani ni muhimu kwa taasisi za kifedha kutumia teknolojia ili kutoa suluhisho za kibunifu ambazo zinakidhi mahitaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Standard Chartered Tanzania Herman Kasekende yeye amesema wanayofuraha kuzindua Straight2Bank Next Gen nchini Tanzania, kwani ni hatua kubwa katika safari yao ya mageuzi katika mifumo ya kidijitali.
“Sisi kama benki, tumejikita katika utoaji wa suluhu za kiubunifu zinazoendeshwa na teknolojia, ili kukidhi mahitaji ya kila siku ya wateja wetu, na kuhakikisha wanastawi,” Amesema.
Hata hivyo amesema benki yao imedhamiria kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara, huku akieleza kwamba kwa kuzinduliwa kwa ‘Straight2Bank Next Gen,’ ni kutekeleza ahadi yao, kwani mfumo huo umerahisisha upatikanaji wa usalama wa huduma zao za kibenki ili kuwasaidia wateja wao kuzingatia kile ambacho ni muhimu zaidi katika kukuza biashara zao.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Benki (Transaction Banking wa Standard Chartered) Afrika Mashariki, Makabelo Malumane amesema sababu iliyowapelekea kuanzisha mfumo huo ni kuhakikisha wateja wao wananufaika na huduma zao kwa haraka na kwa njia nafuu.
“Tumekuwa tukipokea maoni mbalimbali kwa wateja wetu kuhusu mifumo yetu tofauti tulioianzisha, wengine wakihitaji uboreshwaji wa baadhi ya mfumo yetu, hivyo ndio maana tukaamua kuja na mfumo huu mpya ambao utakua msaada kwa makampuni mbalimbali nchini hapa” amesema.
Straight2Bank Next Gen imeundwa kwa kutumia uzoefu mkubwa wa Standard Chartered wa kidijitali, ili kuwawezesha wateja kupata huduma za kifedha za kidigitali ambazo zinarahisisha ufanyaji wa biashara zao.
Mfumo huu wa kibenki kidijitali sasa unapatikana kwa wateja wote wa makampuni nchini Tanzania, huku wateja wakihamasishwa kuutumia mfumo huo ili kufikia malengo yao ya biashara