Bila vyanzo mbadala umeme maumivu nchini

Muktasari:

Mabadiliko ya tabianchi yaliyopunguza megawati 345 za umeme unaozalishwa nchini, yamewaamsha wadau wa nishati wakishauri vitumike vyanzo mbadala kutatua changamoto hiyo wakati wowote itakapojitokeza.

Dar es Salaam. Mabadiliko ya tabianchi yaliyopunguza megawati 345 za umeme unaozalishwa nchini, yamewaamsha wadau wa nishati wakishauri vitumike vyanzo mbadala kutatua changamoto hiyo wakati wowote itakapojitokeza.

Wadau hao wamesema Tanzania imejaaliwa vyanzo vingi vinavyoweza kutumika kuzalisha nishati hiyo badala ya kutegemea tu mafuta na nguvu za maji.

Kwa mujibu wa wadau hao, nje ya vyanzo hivyo, siyo tu ni muhali kwa Tanzania kuwa na uhakika wa umeme kwa siku zote, bali nchi inaweza kukumbwa na maumivu ya mara kwa mara ya kukosa nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Pamoja na wasiwasi uliopo sasa, ripoti ya Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) inaonyesha uwezekano wa mabadiliko zaidi katika siku za usoni iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa.

Ripoti hiyo ya Oktoba inasema hadi mwaka 2030 kutakuwa na athari nyingi zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi Afrika, ukiwamo ukame katika baadhi ya maeneo.

Katibu Mkuu wa WMO, Petteri Taalas anasema viashiria vya hali ya hewa barani Afrika mwaka jana vilionyesha joto litaongezeka, kina cha bahari kitapanda na kutakuwa na ukame katika baadhi ya maeneo.

Kufikia muda huo, ukame utawaathiri takriban watu milioni 118 wanaoishi katika umaskini.

Majanga mengine watakayokumbana nayo watu hao ni mafuriko na joto kali, hali itakayoathiri maendeleo na jitihada za kupunguza umaskini na kukuza uchumi.

Ni kutokana na madhara kama hayo, baadhi ya vyanzo vya umemee, hasa maji, vitaathirika moja kwa moja na ndiyo maana wadau wanashauri njia mbadala.


Gesi asilia

Mojawapo ya chanzo mbadala cha umeme ni gesi asilia, ambayo Abdulsamad Abdulrahim, mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), anasema ipo hazina kubwa inayoweza kumaliza tatizo la umeme.

“Kukatika kwa umeme ni tatizo la siku nyingi, lakini hatujavitumia vyanzo mbadala vilivyopo, hasa gesi asilia. Licha ya hazina kubwa ya gesi tuliyonayo, tukichanganya vyanzo vya umeme kwa kujumuisha jua, upepo na mawimbi ya bahari tutalimaliza tatizo lililopo,” alisema Abdulrahim.


Jotoardhi

Mbali na gesi asilia ambayo imeshaanza kutumika kwa kiwango kidogo hapa nchini, vilevile upo uwezekano wa kuzalisha umeme kwa kutumia jotoardhi.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Kato Kabaka anasema upo uwezekano wa Tanzania kuzalisha megawati 5,000 kutokana na jotoardhi katika vyanzo vilivyothibitishwa katika mikoa 16 nchini.

Jotoardhi hutokana na joto la asili la dunia lililopo chini ya ardhi katika mfumo wa majimoto, mvuke au miamba mikavu, hasa katika sehemu zilizopitiwa na Bonde la Ufa. Iwapo wataalamu watapatikana, anasema Tanzania itanufaika na rasilimali hiyo ya uhakika.


Umeme jua, upepo

Jana gazeti hili lilikuwa na habari kuhusu Kampuni ya Total Energies ikieleza kuwa ipo tayari kuzalisha kiasi chochote cha umeme ambacho Serikali itakihitaji kwa kutumia umemejua na nguvu za upepo.

Kampuni hiyo ilisema inao uzoefu wa kutosha katika eneo hilo kwa kuwa tayari inazalisha umeme katika mataifa tofauti duniani, hususan barani Ulaya na Uarabuni kwa kutumia jua, upepo na joto ardhi.

“Sasa ni wakati wa Tanzania, tunaiona fursa kwenye jua na upepo,” alisema mkurugenzi wa sheria na uhusiano wa kampuni hiyo, Getrude Mpangile.

Hivi sasa kampuni ya Total Energies inatekeleza mradi wa umemejua huko Al Kharhsaah nchini Qatar unaotarajia kuzalisha megawati 800, ukigharimu Sh1 trilioni.

Iwapo mradi kama huo ungetekelezwa nchini, kwa kutumia bajeti ya Sh6.5 trilioni iliyoelekezwa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), Tanzania ingepata zaidi ya megawati 5,200 badala ya megawati 2,115 zinazotarajiwa.

Kutokana na mradi huo unaotekelezwa kwa ubia kati ya Total Energies na Kampuni ya Marubeni ya Japan, wananchi watanunua uniti moja kwa Sh36.04, huku viwanda na watumiaji wengine wakubwa vikilipia Sh75.9 kwa uniti moja.

Gharama za umeme

Hata hivyo, Novemba 18, 2020, aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dk Merdard Kelemani alisema “gharama za kuzalisha umeme wa maji ni ndogo, yaani Sh36 tu kwa uniti.”

Alisema umeme wa gesi ni Sh147 kwa uniti, umeme wa mafuta mazito ni Sh256 kwa uniti mpaka Sh500 na vyanzo vingine hivyo hivyo.

Serikali inawakaribisha

Serikali kwa upande wake inasema haina pingamizi kwa wawekezaji wa vyanzo mbadala vya umeme ikiwa watafuata masharti.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Leonard Masanja alisema mwekezaji anachopaswa kufanya ni kuainisha mpango wake na kuwasiliana na Tanesco na wizara.

“Uwekezaji kama huo unategemea makubaliano, hususan kwenye masuala ya fedha. Wapo wanaotaka wazalishe umeme waiuzie Tanesco au waanzishe mradi kisha Serikali irudishe gharama kama mkopo na kuna wanaotaka mradi wa pamoja na Serikali,” alisema.

Kwa mujibu wa Masanja, kipaumbele cha Serikali ni kuwekeza kwenye miradi ya umeme ili kupata umeme wa kutosha na kuwa upungufu wa maji uliopo sasa, hautoshi kuthibitisha kuwa umeme wa maji haufai.


Mpango wa Serikali

Akizungumzia mikakati ya Serikali kuhusu umeme, Masanja alisema wanaitumia zaidi ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 inayoeleza mipango hiyo katika ukarasa wa 103.

Ilani hiyo CCM inaeleza kwa miaka mitano ijayo, Serikali itaimarisha sekta ya nishati kwa kuhakikisha nchi inazalisha umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda na soko la nje. “Katika kufikia azma hii, CCM itakamilisha ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115, kukamilisha ujenzi wa mradi wa Kinyerezi I – Extension wa megawati 185 na mradi wa umeme wa maji wa Rusumo wa megawati 80),” inasomeka ilani hiyo.

Vilevile ilani hiyo inasema Serikali itaongeza uwezo wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu, ikiwemo miradi ya umemejua, jotoardhi na upepo kupata megwati 1,100.

Katika ilani ya uchaguzi wa mwaka 2015, CCM ilisema kipaumbele kingekuwa kuzalisha umeme utokanao na makaa ya mawe, maji, gesi asilia na nishati jadidifu ili mpaka mwaka 2020 ziwe zinazalishwa megawati 4,915 kutoka megawati 1,308 zilizokuwa zinapatikana mwaka 2015.

“CCM itaielekeza Serikali kuongeza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa nishati ili kukuza sekta hiyo na kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma hii kulingana na sera ya nishati ya Taifa na kutekeleza miradi iliyoainishwa kwenye mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya umeme ya mwaka 2009 mpaka mwaka 2033),” inasomeka ilani hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Jimbo la Manonga, Seif Gulamali alisema muhimu ni kuwa na vyanzo tofauti na maji ambayo bado ni chanzo kizuri, ndiyo maana nchi nyingi zinaendelea kuutumia umeme wake.

Kutokana na upungufu wa umeme uliopo nchini, Novemba 17, Waziri wa Nishati, January Mkamba alizungumza na Balozi wa Dernmark nchini, Mette Norgaard Dissing Spandet na kuwakaribisha wawekezaji wenye uwezo kuwekeza kwenye umeme jadidifu nchini.

Balozi Spandet alisema wawekezaji kutoka Denmark wapo tayari kuja kuzalisha umeme wa upepo ambao Baraza la Kimataifa la Nishati ya Upepo (GWEC) linasema mpaka mwaka 2020 megawati 743,000 zilikuwa zinatokana na chanzo hicho duniani.


Maoni mbadala

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema ili kuwa na suluhisho la kudumu la umeme ni muhimu kufanya mabadiliko, maeneo ya uzalishaji na usambaji wa umeme yawe na kampuni tofauti.

“Tanesco inapaswa kuwa na kampuni tanzu tatu, ya uzalishaji, usafirishaji na ya usambazaji, ya uzalishaji na usambazaji iwe inashindana na sekta binafsi, lakini ya usafirishaji ibaki ni ya umma tu,” alisema Zitto.

Alisema kwa sasa matatizo ya umeme yanayotokea ni kwa sababu ya kutokufuata mipango ya nchi kwa mujibu wa taratibu kwa kuwa kuna mpango kabambe wa umeme na kama ungetekelezwa ulivyo leo kungekuwa na umeme wa ziada.

Alisema mpango huo ulivurugwa mwaka 2017 baada ya Serikali kuelekeza nguvu zake kwenye mradi wa umeme wa Mto Rufiji ikiamini ndilo jawabu la kudumu na kusahau kutafuta majibu ya muda mfupi.

“Ukame ulivyotokea maji hakuna, bwawa halijaisha, uwekezaji wa gesi umesimama, miradi yote ya upepo wa jua imesimama na si kwamba haikuwepo, kulikuwa na mipango, changamoto ni kwamba iliwekwa pembeni, cha kufanya sasa ni kutekeleza mpango kabambe wa umeme,” alisema Zitto.

Alisema matatizo ya umeme yaliyopo hivi sasa ni makosa ya kibinadamu si makosa ya Mungu na suluhisho la muda mfupi, Serikali iharakishe uwekezaji wa sekta binafsi kwenye miradi iliyo tayari ya upepo, mradi mkubwa wa sola kwa maeneo hayo mawili ndani ya mwaka mmoja tutapata MW450 za umeme.