Bilionea aliyeanzia kuuza tairi chakavu, kukodisha walinzi

Muktasari:

  • Katika matoleo mawili yaliyopita tulisimulia maisha ya utotoni, ujanani na ndoa ya Roman Abramovich. Tajiri huyo ni yatima aliyelelewa katikika umaskini wa kupitiliza, lakini baadaye maishani akafanikiwa kuwa mmoja wa matajiri wakubwa zaidi duniani.

Katika matoleo mawili yaliyopita tulisimulia maisha ya utotoni, ujanani na ndoa ya Roman Abramovich. Tajiri huyo ni yatima aliyelelewa katikika umaskini wa kupitiliza, lakini baadaye maishani akafanikiwa kuwa mmoja wa matajiri wakubwa zaidi duniani.

Tulisimulia pia kuwa katika ujana wake Abramovich aliwahi kujiunga na jeshi kwa muda mfupi sana kabla ya kuacha na kuanza kujitafutia kipato. Akiwa Moscow alijiunga na kozi ya masuala ya mafuta na gesi katika taasisi ya Gubkin Institute of Oil and Gas ambako alikuwa anasoma huku akiuza matairi chakavu ya magari kujikimu kimaisha.

Akiwa anapambana na maisha huko Moscow mwaka 1987, alikutana na Olga Lysova ambaye baadaye alikuja kuwa mkewe.

Olga alikuwa ni mwanamke mwenye kuvutia kutoka jiji la Astrakhan nchini humo, aliyekuwa akisoma jiolojia katika chuo cha Ukhta.

Akiwa na umri wa miaka 23, si tu kwamba alikuwa amemzidi Abramovich kwa miaka mitatu pia tayari alikuwa na binti mdogo aliyezaa kwenye ndoa yake ya awali. Abramovich na Olga walikutana kwenye baa na, Olga anakumbuka kwamba Abramovich alikuwa na haya kiasi kwamba hakumkabili moja kwa moja bali alimtuma rafiki yake amwombe wacheze muziki.

Baadaye Olga alikaririwa na jarida la ‘News of the World’ akisema: “Nilikubali (kucheza) na alinivutia mara moja. Roman (Abramovich) alikuwa mwanamume mtanashati, mrefu,mwembamba, mwenye macho ya bluu yanayovutia na alikuwa amevalia vizuri sana.

“Alivaa suti kila wakati, hata nyumbani. Tulicheza kwa wimbo wa polepole wa pop wa Kirusi. Alicheza vizuri nilijiruhusu anishike mikononi mwake na akaniongoza kucheza ... Ilikuwa ni neema ya kipekee. Tuliongea na kuongea.

“Alionekana kuwa mzito sana na mtu mzima kwa umri wake. Tulitoka baa pamoja na kuketi usiku kucha tukizungumza na kumbusu.

Nilimwambia tayari nilikuwa nimeolewa na nina binti mwenye umri wa miaka mitatu, Anastasia. Aliniambia anapenda watoto na kwamba binti yangu hangekuwa tatizo kwake. Tena nilivutiwa na ukomavu wake.”

Wenzi hao walioana kimya kimya Disemba 1987 katika ofisi ya usajili wa ndoa ya Dzerzhinski huko Moscow mbele ya familia na marafiki 15 tu, na waliishi pamoja katika chumba kimoja cha ghorofa chenye ukubwa wa mita 18 za mraba ambacho Abramovich alikuwa ameachiwa na marehemu bibi yake.

Tangu mwanzo mambo hayakuwa rahisi kwa wenzi hao wachanga.

Kwa muda mrefu Abramovich alikuwa anapungukiwa fedha na kumuomba rafiki yake aliyeitwa Svetlana Suetina kumlipia chakula au kumnunulia vyakula vya msingi kama vile nyama. Baada ya muda, alihama kutoka Taasisi ya Ukhta kwenda Taasisi ya Usafiri wa Barabara ya Moscow, ambapo alitunukiwa diploma.

Na baada ya miaka kadhaa huko Moscow, alikuwa na mafanikio ya kutosha kumpeleka ‘Sveta’ (Olga) kama alivyomwita kwenda kupata mlo wa gharama kubwa kwenye mkahawa ambao ulitajwa kama ‘mahali ambapo huenda makahaba tu na watu wasio na mapato’.

Hata hivyo, ndoa ya Abramovich na Olga ilidumu kwa miaka mitatu tu, kutoka 1987 hadi 1990. Kufikia wakati huu wa kutengana kwao, Abramovich alikuwa amechoka maisha ya kusomea uhandisi wa barabara katika taasisi ya Ukhta.

Hizi zilikuwa ni zile siku za mwisho za vita ambapo Alhamisi ya Disemba 26, 1991 Umoja wa Soviet ulisambaratika na kwa kiasi fulani kuanzia hapo, ubebari ukaanza kuchomoza ingawa kwa mbali.

Hapa ndipo Abramovich alianza kufanya biashara ya kila namna. Kwa muda mrefu alikuwa akijiongezea kipato kwa kununua bidhaa kama sigara, manukato na biskuti huko Moscow na kuzisafirisha kwa ndege hadi Ukhta na kuziuza tena kwa faida.

Alianzisha pia biashara ya kuuza midoli, matairi chakavu za magari. Baadaye aliibadili biashara ya tairi chakavu na kuwa wakala wa matairi mpya kutoka viwandani. Kuanzia 1992 hadi 1995, Abramovich alianzisha kampuni tano katika sekta ya mafuta na kuwa mmiliki mwenza wa kampuni moja kubwa ya mafuta iitwayo ‘Sibneft’. Pia alinunua hisa katika kampuni kadhaa.

Biashara iliyomkutanisha na watu wengi ni ya kutoa ulinzi binafsi. Wakati anaanza maisha yake jijini Moscow yakiwa yamemwendea vibaya, aliwahi kufanya kazi ya ulinzi binafsi. Lakini baadaye aliamua kuanzisha kampuni na kukusanya vijana wa kuifanya.

Kipindi ambacho ujamaa unaanguka mwanzoni mwa miaka ya 1990, Serikali ilibinafsisha nyenzo zake za kiuchumi kwa watu wachache.

Kwa kuwa hao watu wachache walitamani sana nyenzo hizo ili kujipatia mali, waliviziana kwa kudhuriana na hata kuuana ili kupata mali.

Katika mazingira kama haya ambapo miili ya matajiri, waandishi wa habari na hata viongozi wa kisiasa kila mara ilikuwa inakutwa imetupwa mitaani, hivyo biashara ya ulinzi binafsi ikashamiri.

Matajiri walikuwa na hofa na maisha yao muda wote, kwa hiyo walihitaji ulinzi wakati wote.

Kazi za kuwalinda matajiri na biashara zao zilimfanya Abramovich kujuana na watu muhimu ndani na nje ya jiji la Moscow.

Miongoni mwa watu hawa muhimu ambao baadaye walikuja kuwa kama ‘mshauri’ wake wa maana sana maishani ni Boris Berezovsky.

Huyu alikuwa mhadhiri wa chuo kikuu lakini akaacha kufundisha na kugeukia biashara ili asipitwe na upepo wa utajiri uliokuwa unavuma Urusi kipindi hicho, wakati nchi hiyo ilipotekeleza sera ya ubinafsishaji wa mali za Serikali.

Berezovsky alikuwa ni mmoja wa matajiri wa kwanza kwanza kabisa ndani ya Urusi ulitokana na kunufaika sana na ubinafsishaji wa mali za umma. Mojawapo ya biashara za awali za Berezovsky ilikuwa kampuni iliyoitwa ‘All-Russia Automobile Alliance’ (AVVA) aliyoianzisha mwaka 1993 akiwa na Alexander Voloshin (Mnadhimu Mkuu katika Serikali ya Boris Yeltsin).

Berezovsky alidhibiti takribani asilimia 30 ya hisa zote za kampuni hiyo. Hawa walijenga kiwanda cha kutengeneza magari. Zaidi ya hilo, Berezovsky alikuwa miongoni mwa watu wachache sana ambao walikuwa karibu na Rais wa Russia kipindi hicho, Boris Yeltsin. Watu hawa walikuwa ni wanafamilia wa Yeltsin pamoja na matajiri wachache sana walijiita ‘The Family’.

Kikundi hiki cha matajiri wachache pamoja na familia ya Rais ndio walikuwa wanaendesha nchi na waliitwa ‘oligarch’.

Kwa hiyo kitendo cha Abramovich kujiweka karibu na Berezovsky kilimaanisha kwamba alikuwa amefanikiwa kujenga urafiki na mmoja wa watu muhimu zaidi nchini Russia, mwenye ushawishi ndani ya kikundi cha matajiri waliomzunguka Rais.

Baada ya urafiki Abramovich na Berezovsky kukomaa na kushibana. Abaramovich alimuomba Berezovsky amsaidie kumtambulisha kwa watu muhimu Kremlin.

Moja kwa moja Berezovsky akahisi labda Abramovich anataka kutambulishwa kwa Rais au mawaziri na akamjibu bado hajafikia ngazi ya kutambulishwa kwa watu hao.

Lakini Abramovich akamwambia hahitaji kutambulishwa kwa Rais au mawaziri bali kwa mtu anayeitwa Valetin Yumachev.

Je, huyu Valetin Yumachev ni nani? Fuatilia kesho kujua zaidi.