Bilioni 4.7 kuondoa adha ya maji Kyela

Tuesday May 17 2022
kyela pic
By Hawa Mathias

Kyela. Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa zaidi ya Sh4.7 bilioni kwa ajili ya kuboresha mradi mkubwa wa maji kutoka katika chanzo cha Mto Mambwe Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya utakaohudumia wananchi 58,000.

Meneja  Ufundi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (Mbeya Uwwas), Mhandisi Barnabas Konga amesema hayo wakati wa kukabidhi mradi wa maji  wenye thamani ya zaidi ya Sh197 milioni kwa Meneja wa Ruwasa, Tanu Deule uliojengwa katika kijiji cha kingiri halmashauri ya Wilaya ya Busokelo Wilaya ya Rungwe

''Kuna miradi ya Maji ambayo kwa miaka mingi imekwama kuendelea Wizara ilirejesha kwa Mamlaka za Maji nchini ambapo kwa Mkoa wa Mbeya na Songwe kuna miradi 15 ambayo ilirejeshwa na yote imetekelezwa na kukabidhiwa katika halmashauri husika ''amesema Mhandisi Konga.

Kuhusu mradi wa mto Mambwe ambao utekelezaji wake unaendelea amesema kwa sasa umefikia hatua nzuri na ukikamilika utaondoa adha ya maji katika kata, vijiji, tarafa zote Wilaya ya Kyela.Advertisement

''Mradi huo umenza mwaka 2021  kwa sasa uko katika hatua za utandikaji wa mabomba na uboreshwaji wa miundombinu ya usafirishaji wa maji na umefikia  hatua nzuri  lengo la Wizara kutoa fedha ni kuwezesha jamii kuondokana na hadha ya maji iliyodumu kwa miaka mingi na kumtua mama ndoo kichwani.''amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Ismail Mlawa ameiomba Wizara ya Maji kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo kutokana na maji yanayotumiwa na wananchi kutokuwa salama kwa afya zao hususan ya visima na mifereji.

''Wilaya ya Kyela ina changamoto kubwa ya maji hivyo niombe tu Mamlaka Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya kushirikiana na Ruwasa kutekeleza miradi ya maji ikiwa ni pamoja na kudhibiti uharibifu wa Mazingira unao tokana na shughuli za kijamii ''amesema.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Kyela, Tanu Deule amewataka wananchi kutoingia na kugfanya shughuli za kilimo na ufuhgaji katika vyanzo hivyo.

Mkazi wa kijiji cha Kingiri, Subiraga Mwakyusa amesema kuwa kumekuwepo na changamoto ya uchafuzi wa mazingira katika vyanzo vya maji jambo ambalo linahatarisha usalama wa watumiaji maji kupata maradhi kutokana na kuwepo kwa vinyesi vya ng'ombe.

Advertisement