Biteko aipongeza Barrick

Biteko aipongeza Barrick

Muktasari:

Julai 2019 kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania walitiliana saini makubaliano ya uendeshaji wa migodi ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi uliofuatiwa na kuundwa kwa kampuni ya madini ya Twiga Oktoba,2019.

Mwanza. Waziri wa Madini, Dotto Biteko ameipongeza kampuni ya Barrick kwa kutekeleza sheria na kanuni zinazoelekeza kampuni za ndani na Watanzania kupewa zabuni  kutoa huduma katika migodi.

Akizungumza na watendaji wakuu wa kampuni hiyo jijini Mwanza leo Alhamisi Februari 25, Biteko amesema pamoja na kuipa Serikali ya Tanzania Dola 100 milioni (Sh231 bilioni) ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya malipo ya Dola 300 milioni, kampuni hiyo pia imetoa zabuni ya zaidi ya Dola 290 milioni kwa kampuni za ndani kupita sheria na kanuni.

"Fedha hizi zimelipwa kwa kampuni za ndani na kuingia kwenye mzunguko na uchumi wa ndani," amesema Biteko.

Biteko ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wawekezaji wa ndani na nje juu ya utayari wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi kukuza uchumi unaonufaisha na kujali maslahi ya pande zote.

Awali, Rais na ofisa mtendaji mkuu wa Barrick, Mark Bristow ameihakikishia Serikali na Watanzania uwepo wa nia thabiti wa kuongeza uzalishaji na hatimaye faida katika migodi ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi ambayo kwa pamoja inaendeshwa  kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga.

Ofisa Mtendaji mkuu huyo amesema kwa kuzingatia muktadha huo, uongozi wa juu wa Barrick upo nchini kwa mkutano wa kikazi wa kupanga mikakati ya utendaji.