Biteko azuia uongozi Tanesco kushiriki kongamano la nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza katika moja ya mikutano ya wizara hiyo.
Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewazuia viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhudhuria Kongamano la Kimataifa la Nishati linaloendelea muda huu jijini Dar es Salaam na badala yake kufuatilia changamoto za kupunguza maumivu ya upatikanaji wa umeme nchini.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameagiza viongozi waandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kufuatilia changamoto za upatikanaji wa umeme badala ya kuhudhuria Kongamano la Kimataifa la Nishati linaloendelea muda huu jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo kwa awamu ya tano limekutanisha mamia ya watalaamu wa nishati, kampuni za mafuta, nishati, gesi, nishati jadidifu na taasisi za umma litaendesha mijadala mbalimbali kutafuta mbinu na mtazamo ya uwekezaji wa nishati jadidifu pamoja na nishati safi ya kupikia.
Akizungumza katika hotuba yake kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Dk Biteko amesema; “Tuko hapa leo tunajadili nishati, ukizungumzia nishati kwa Watanzania wanaelewa ni umeme,” amefafanua.
“Rais (Samia Suluhu Hassan), Makamu wa Rais (Dk Philip Mpango) na wewe (Waziri Mkuu Kassim Majaliwa), mmenielekeza kwa muda mrefu toka nimeteuliwa kwamba, tufanye kila tunaloweza kuhakikisha maumivu ya upungufu wa umeme tunayamaliza.”
“Tunafahamu ya kwamba ukuaji uchumi ni mkubwa kwa watu wetu lakini vyanzo vyetu vya umeme bado ni vile vile, lazima tuongeze vyanzo vipya ili kuwa na uhakika kwa ajili ya shughuli zetu za kiuchumi, jana tu ripoti ilitolewa ikionyesha katika nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi, Tanzania tumo,” amesema.
“Maana yake ni kwamba mahitaji ya umeme yataendelea kuwepo, ndiyo maana mheshimiwa Waziri Mkuu utaona katika mkutano huu baadhi ya watu wetu wa wizarani, tumewaambiwa wala hapa (katika kongamano), msije kwa sababu sisi tunataka umeme,” ameeleza Biteko.
“Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco hatawepo pamoja na wenzake, kwa siku tatu tunajaribu kuangalia wapi tuta-push in (kusukuma), ili makali ya upungufu wa umeme tuweze kuyakabili. Kwa hiyo niwatoe wasiwasi Watanzania wenzangu, hili ni jambo la mpito wakati Bwawa la Mwalimu Nyerere likikamilika,” amesema.