Biteko: Wananchi shirikini miradi ya maendeleo

Mbunge wa jimbo la Bikombe mkoani Geita. Dk Doto Biteko akihamasisha wananchi kuchagia  malizao na nguvu kwenye mirafi ya maendeleo wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara kijiji cha Ihulike kata ya Ushirombo huku akiongeza kuwa hakuna nchi duniani iliyo endelea bila michango ya wananchi, Picha na Ernest Magashi.

Muktasari:

  • Wananchi wilayani Bukombe wametakiwa kushiriki kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuchangia nguvu ili kufanikisha malengo ya Serikali kuboresha huduma za jamii.

Bukombe. Wananchi wilayani Bukombe wametakiwa kushiriki kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuchangia nguvu ili kufanikisha malengo ya Serikali kuboresha huduma za jamii.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Bukombe, Doto Biteko ambaye ni waziri wa madini pia aliposikiliza kero za wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ihulike kilichopo Kata ya Ushirombo.

Dk Biteko amesema hakuna nchi iliyopata maendeleo bila kushirikisha nguvu za wananchi.

Licha ya wito huo, Biteko ametoa mabati 220 yenye thamani ya Sh6.4 milioni na matofali 2,000 ya Sh2.2 milioni kufanikisha ujenzi wa Zahanati ya Ihulike pamoja na mifuko 50 ya saruji yenye thamani ya Sh1.1 milioni kusaidia ujenzi wa Shule Shikizi ya Msingi Shikalibuga na Sh1 milioni za kukamirisha choo cha wanafunzi wa Shule ya Msingi Kuziba.

"Namushukru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za maendeleo jimboni  kwetu, miradi mingi itakamilika ukiwamo wa kuongeza maji mjini Ushirombo na madarasa yote yaliyojengwa yatakamilika na kujenga mengine mapya ili kukabili uhaba wa madarasa ndani ya Wilaya ya Bukombe," amesema Biteko.

Akielezea athari za janga la Uviko-19 amewataka Wanabukombe kuendelea kuchukua tahadhali dhidi ya ugonjwa huo hatari ikiwamo kuchanja.

Awali, Diwani wa Ushirombo, Lameck Warangi alisema msada wa saruji na mabati aliyotoa mbunge wao watafanikisha malengo ya kukamilisha miradi hasa ya afya iliyochelewa kutokana na wananchi kutokuwa tayari kuchangia tangu mwaka 2017.

Kata ya Ushirombo, amesema haina kituo cha afya ila ina zahanati moja ambako wananchi hulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma zake.

Warangi amempongeza Biteko kwa kufanikisha kuchongwa kwa barabara yenye urefu wa kilomita 24 ndani ya Kata ya Ushirombo itakayosaidia kupunguza zilizokuwapo kutokana na ubovu wa miundombinu hiyo uhimu.