Bosi wa Equinor atua nchini kufuatilia mradi wa LNG

Muktasari:

Makamu wa Rais wa kampuni ya Equinor iliyowekeza kwenye mradi wa kusindika gesi asilia (LNG), Nina Koch ametua nchini kuangalia maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya dola 30 bilioni za Marekani (takriban Sh70 trilioni).

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa kampuni ya Equinor iliyowekeza kwenye mradi wa kusindika gesi asilia (LNG), Nina Koch ametua nchini kuangalia maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya dola 30 bilioni za Marekani (takriban Sh70 trilioni).


Amewasili nchini leo Alhamisi Desemba 8, 2022 akitokea Norway yalipo makao makuu ya kampuni yake, Nina amepokelewa na kuzungumza na Waziri wa Nishati, January Makamba kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.


Katika kikao hicho, Nina na Makamba wamezungumzia maandalizi ya mradi na kubainishwa kuwa timu za majadiliano kutoka serikalini na upande wa wawekezaji zipo katika hatua ya uandishi (drafting) wa mikataba ya mwisho (final agreements) baada ya makubaliano katika mambo yote ya msingi kufanyika Novemba 2022.

Nina amesema Equinor ipo tayari kutoa ushirikiano unaohitajika kujenga ofisi maalum ya mradi wa LNG itakayosimamia na kuratibu shughuli za mradi katika kipindi cha ujenzi na uendeshaji.

"Mradi huu ni muhimu na umepokelewa kwa mtizamo chanya nchini Norway. Kwa uzoefu wangu miradi kama hii sio rahisi kukubalika moja kwa moja na pande zote yaani kampuni na Serikali lakini kwa huu, Serikali na wananchi wa Norway wanauunga mkono,” amesema Nina.

Katika ziara hiyo, Nina ametembelea eneo utakapojengwa mradi huko mkoani Lindi na ameipongeza Serikali kwa kuchagua karibu na uwanja wa ndege jambo litakalorahisisha usafiri wa wafanyakazi na vifaa vitakavyotumika wakati wa ujenzi na uendeshaji wa mradi.

Vilevile, Nina ametembelea Chuo cha Veta Lindi kinachofadhiliwa na kampuni zinazotarajiwa kuwekeza katika mradi huo wa LNG.

Katika ziara hiyo ambayo Nina ameongozana na Mkuu wa Kitengo cha Mkondo wa Juu Kimataifa wa Equinor, Nizar Damree, Makamu wa Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Equnor Tanzania, Unni Fjær pamoja na Genevieve Kasanga, ofisa mawasiliano Equinor Tanzania amemweleza Waziri Makamba kuwa wataendelea na kuvifadhili vyuo hasa vilivyopo mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuwajengea uwezo Watanzania kushiriki kuanzia ujenzi mpaka uendeshaji wa mradi wa huo.

Kwa upande wake, Waziri Makamba ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika mazungumzo yanayoendelea kati ya wawekezaji na Serikali na akasisitiza kuwa "natarajia mradi utatekelezwa kwa wakati kama ilivyopangwa."

Katika kikao hicho, Waziri Makamba aliambatana na Kamishna wa Mafuta na Gesi wa Wizara ya Nishati, Mike Mjinja pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Charles Sangweni.

Utekelezaji wa mradi huu sio tu utasaidia kuipa Tanzania nishati safi bali utakuza Pato la Taifa na kuimarisha thamani ya shilingi na mzunguko wa fedha kutokana na mauzo ya nje ya gesi hiyo asilia.

Mazungumzo ya utekelezaji wa mradi huo yalianza katika Serikali ya awamu ya nne lakini yasimama kwa muda kabla hayajafufuliwa na Rais Samia Suluh Hassan.