Bosi wa zamani MSD afutiwa kesi ya uhujumu uchumi

Bosi wa zamani MSD afutiwa kesi ya uhujumu uchumi

Muktasari:

  • Bwanakunu na Tabura amefutiwa mashitaka baada ya kukaa mahabusu kwa takribani siku  341 kabla ya DPP kuamua kutoendelea na mashitaka dhidi yao.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu.

Mbali na Bwanakunu, mwengine aliyeachiwa ni aliyekuwa Kaimu  Mkurugenzi wa Logistiki wa MSD, Byekwaso Tabura, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania  (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.

Bwanakunu na Tabura walikuwa wanakabiliwa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matano, yakiwemo ya kuisababishia MSD hasara ya Sh 3.8bilioni na kutakatisha fedha kiasi cha Sh 1.6 bilioni.

Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka hayo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai  (CPA), sura ya 20  iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Uamuzi huo umetolewa leo, Mei 13, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Kassian Matembele baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, ameieleza mahakama kuwa hati hiyo ilisainiwa Mei 10, 2021 na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania ( DPP), Biswalo Mganga, ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Amedai kuwa hati hiyo ilisainiwa chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2019.

Simon baada ya kueleza hayo, Hakimu Matembele amesema kupitia kifungu hicho, mahakama imewafutia mashtaka washtakiwa hao wawili na imewaachia huru.

Hakimu Matembele amesema kupitia kifungu hicho, DPP anao uwezo wa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka, washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2016 na June 30, 2019 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa makusudi washtakiwa aliongoza genge la uhalifu

Shtaka jingine ni kuisababishia hasara MSD, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Julai mosi, 2016 na June 30, 2019, katika eneo la MSD lililopo Keko, washtakiwa waliisababishia MSD hasara ya Sh 3.8 bilioni.