BOT yaombwa kubadili sera ya mikopo kwa wajasiriamali

Muktasari:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetakiwa kupitia na kuirekebisha sera ya mikopo kwa wafanyabiashara wadogo ili iwe rafiki na iweze kutimiza malengo ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.

Arusha. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetakiwa kupitia na kuirekebisha sera ya mikopo kwa wafanyabiashara wadogo ili iwe rafiki na iweze kutimiza malengo ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.

Hayo yamesemwa na mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe alipotembelea mabanda ya BOT  katika maonesho ya 28 ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yanayoendelea katika viwanja vya Themi mkoani Arusha.

Amesema  sera ya taasisi za kifedha iliyopo kwa wafanyabiashara wadogo inayowataka kuanza kulipa marejesho ya mkopo baada ya mwezi mmoja toka siku ya kuichukua sio rafiki kwani inawaweka wajasiriamali katika mateso makubwa ya kutafuta njia ya kulipa.

“Unakuta umemkopesha mtu fedha leo baada ya siku 30 unataka aanze kurejesha, hivi kama ni biashara au ameiingiza katika ujasiriamali imetosha kutoa faida ya kulipa mkopo huo? Matokeo yake anajikuta anauza kile alichonacho alipe rejesho kitendo ambacho hakiwezi kumnyanyua kiuchumi," amesema Mwaisumbe.

Amebainisha kuwa ili uchumi ukue kwa kasi ni lazima wafanyabiashara wadogo wanufaike na kazi zao na kuwataka BOT kuwasiliana upya na taasisi zake za fedha kupunguza mikopo chechefu kwa kuweka mazingira mazuri ya uwezo wa wakopaji kulipa.

“BOT anzeni sasa kufanya kazi ya kutimiza malengo ya Taifa ya kukuza uchumi, kumkopesha mtu kwa masharti magumu ashindwe  kulipa matokeo yake kumuuzia mali zake au nyumba huko ni kumfilisi na kushusha uchumi hivyo anzeni kutoka mikopo ya mda mrefu kuanzia mwaka”

Awali akitoa maelezo ya mikopo hiyo ofisa mwandamizi wa BOT, John Matinde amesema,  "ili  kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali tunahakikisha taasisi za fedha zinatoa huduma stahiki kwa wateja ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu ili wateja waweze kurejesha”

Naye meneja msaidizi idara ya sarafu tawi la Arusha, Philemon James amesema ili kusimamia ubora wa fedha za Tanzania, BOT iko ukingoni na uchunguzi wa sarafu bandia ya shilingi 500 na watatoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo.

“BOT haina mpango wa kubadili sarafu hiyo kwani tunaamini iko katika kiwango bora na imara hivyo niwatake wananchi wasiikatae kwani iko kihalali na tunaelekea ukingoni katika uchunguzi wetu kwa maofisa walioko mtaani wataleta majibu na siku sio nyingi tutatoa matokeo ya uchunguzi wetu kwa hao wanaotaka kuharibu sifa ya taasisi,” amesema.