Bulaya ataka marekebisho ya sheria ya kikokotoo

Wednesday April 14 2021
By Sharon Sauwa

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Esther Bulaya ameitaka Serikali kupeleka bungeni marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kurekebisha kikokotoo cha mafao ya wastaafu kilichoachwa kiporo tangu mwaka 2018.

Bulaya ametoa kauli hiyo leo  Jumatano, Aprili 14, 2021 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema mwaka 2018 kulitokea sintofahamu ya kikokotoo cha wastaafu ambapo Hayati Rais John Magufuli alisitisha ili kuondoa kasoro zilizoonekana kumnyonya wafanyakazi.

Bulaya amesema katika hotuba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amegusia kuhusu kikokotoo lakini hajaelezea kwa kina kuhusiana na suala hilo.

“Ni  lini mtatatua kisheria suala hili, tuliwaeleza kuwa suala hili litapata ufumbuzi kwa kuleta mabadiliko ya kikotoo bungeni ili yale wanayotaka wafanyakazi juu ya kikokoto chao kilichobeba hatima ya maisha yao yawemo”amesema.

Bulaya amesema waliiambia Serikali kikotoo hicho kiweke kisheria na kisiwe kwenye kanuni zinazoandaliwa na waziri husika lakini hawakusikilizwa na hata wadau pia hawakushirikishwa wakati wa maandalizi ya kanuni hizo.

Advertisement

Amesema matokeo yake walileta kikokotoo kibovu kuliko cha awali, “hivi leo mstaafu anastaafu unampa pesheni asilimia 25 na asilimia 75 utamlipa kidogo haiwezekani. Kwa nini wengine iwe asilimia 75 ama 50 kwa nchi za wenzetu?”

Amesema pia michango ya wafanyakazi imekuwa haipelekwi na ndio maana wastaafu hawalipwi mafao yao.

Ametoa mfano Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF)lina madeni mengi na kwamba shirika hilo linadai Sh 284 bilioni ambazo  haijakusanywa.

Amesema wafanyakazi wana mawazo ya ki kokotoo, michango haijakusanywa, mishahara haijapandishwa na hawajui hatima yao,”amesema.

Advertisement