Bunge lazishtaki taasisi tatu serikalini

Bunge lazishtaki taasisi tatu serikalini

Muktasari:

  • Bunge la Tanzania limeshauri Serikali kuzichukulia hatua taasisi zake nne ili kutilia nguvu sheria ya ukaguzi wa umma.

Dodoma. Bunge la Tanzania limeshauri Serikali kuzichukulia hatua taasisi zake nne ili kutilia nguvu sheria ya ukaguzi wa umma.

 Hayo yamesemwa jana Alhamisi Juni 10, 2021 na Spika wa Bunge,  Job Ndugai wakati akitoa uamuzi wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Ndugai aliiagiza PAC kuyaita mashirika 11 ya Serikali ambayo hayakuwasilisha hesabu zake zilizokaguliwa kwa Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  mwaka 2019.

Akisoma uamuzi huo ameyataja mashirika hayo kuwa ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa Fahamu (Moi), Kampuni ya Mbolea nchini (TFC) na Shirika la magazeti ya Serikali (TSN).

“Tunashauri Serikali kuchukua hatua stahiki kwa taasisi hizo ili kutilia nguvu masharti ya ukaguzi wa umma sura 418,”amesema.

Kuhusu TFC na TSN, Ndugai amesema ushauri wa Bunge baada ya kushindwa kufunga mahesabu yake ni Serikali ifanye tathimini ya kina ili kubaini iwapo mashirika hayo yanatakiwa kuendelea kufanya kazi chini ya mfumo wa sasa au kuyafanyia marekebisho makubwa.

Kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutofunga mahesabu kwa sababu ya kutokuwepo kwa makubaliano ya maandishi kati ya mfuko na Serikali wa ulipaji wa mkopo wa Sh231 bilioni, Bunge limeshauri Serikali na NHIF wakamilishe makubaliano ya kimaandishi.

“Ikiwemo ratiba maalum ya upimaji na kuanza kulipa madeni husika kwa ratiba waliyokubaliana,” amesema,” amesema.

Kuhusu Moi  kutokamilisha mahesabu kutokana na changamoto za mfumo wa kitabibu kutowasiliana ipasavyo na mfumo wa hesabu, wameishauri Serikali ifanye uchunguzi wa mchakato mzima wa ununuzi na usimikaji wa mfumo wa shughuli za kitabibu uliopo Moi.

Amesema lengo la uchunguzi huo ni kubaini kama taratibu zilifuatwa na kama mfumo huo una manufaa kwa Taifa.

Ndugai amesema wanashauri Serikali  ipeleke wataalam wenye sifa  Moi ili kutekeleza shughuli za ukaguzi na uhasibu kwa sababu pameoneka pana shida ya sifa za wahasibu.

Kuhusu kutokamilika kwa wakati kwa  Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL) na Shirika la Posta, amesema wanaishauri ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iboreshe mipango ya ukaguzi na kuzingatia ipasavyo wakati wote wa ukaguzi.

Kuhusu kuongezwa kwa muda wa ukaguzi kwa taasisi tatu zikiwemo Soko la Bidhaa Nchini (TMX), Shirika la Reli Nchini (TRC) na Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT), ushauri ni kuwa ofisi ya Taifa ya Ukaguzi izingatie kwa ukamilifu masharti ya kifungu cha 32 Sheria ya Ukaguzi wa Umma.

“Kinachotoa mamlaka ya kuongeza muda wa ukaguzi kwa Bunge pekee kupitia azimio la Bunge kwa hiyo ni lazima wawe wanafunga hesabu kwa wakati ikibidi waombe kibali na kwa azimio,” amesema.

Ametaka kila taasisi ifunge mahesabu kwa wakati na taarifa ya CAG inapokuja bungeni iwe na taarifa zao.

“Maana nyingine zinajua zitapata hati chafu kwa hiyo zinakwepa wakati wa ukaguzi wanapeleka hesabu zao baada ya ukaguzi huo. Mbinu hiyo tumeigundua, tumestuka..., kama wana busara wajirekebishe,” amesema