Carlos afungwa vifungo vitatu vya maisha -17

Carlos afungwa vifungo vitatu vya maisha -17

Muktasari:

  • Baada ya Jaji Yves Corneloup kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha maisha, Carlos (48, wakati huo) alikuwa na kesi nyingine nne dhidi yake katika nchi nyingine mbalimbali.

Baada ya Jaji Yves Corneloup kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha maisha, Carlos (48, wakati huo) alikuwa na kesi nyingine nne dhidi yake katika nchi nyingine mbalimbali.

Siku moja kabla ya Krismasi, Desemba 24, 1997 Carlos alihukumiwa kifungo cha maisha kwa mauaji aliyoyafanya Ufaransa Ijumaa ya Juni 27, 1975.

Akiwa gerezani, Ijumaa ya Mei 4, 2007 ilijulikana angefikishwa tena mahakamani kwa makosa mengine kadhaa kutokana na mabomu aliyolipua miaka ya 1982 na 1983.

Ugaidi alioufanya mwaka 1982 na 1983 ulisababisha mauaji ya watu kadhaa na zaidi ya 100 kujeruhiwa.

Jaji Jean-Louis Bruguiere aliamuru mashtaka mengine mapya yafunguliwe dhidi ya Carlos ambaye kwa wakati huu alikuwa na umri wa miaka 57.

Mashambulizi ya mabomu aliyoyafanya Carlos katika kipindi hicho ni pamoja na kulipua treni ya mwendo kasi ya kutoka Paris hadi Toulouse.

Katika shambulio hilo lililofanyika Jumapili ya Machi 28, 1982 watu watano walipoteza maisha papo hapo na wengine 28 kujeruhiwa vibaya.

Mwezi mmoja baadaye bomu alilolitega kwenye gari lililipuka mjini Paris likaua mtu mmoja na wengine 60 kujeruhiwa. Gari hilo lilikuwa la kampuni ya gazeti lililoonekana kuipinga Serikali ya Syria.

Kesi hii mpya kuhusu matukio hayo ilianza kusikilizwa Jumatatu ya Novemba 7, 2011 jijini Paris mbele ya Jaji Olivier Leurent. Wakati huu Carlos alikuwa na umri wa miaka 62.

Agosti 25, 1983 alilipua ubalozi mdogo wa Ufaransa huko Berlin Magharibi ambako, kwa mujibu wa kitabu ‘The Black Book of Communism: Crimes, Terror, Repression’ watu wawili walikufa na wengine 23 kujeruhiwa vibaya.

Bomu hilo lililokuwa na uzito wa kati ya kilo 20 na 30, kwa maelekezo ya Carlos lilitegwa katika chumba cha stoo cha jengo hilo kwenye ghorofa ya nne.

Mlipuko huo uliharibu paa la jengo hilo na kusababisha sehemu ya ghorofa ya nne kuanguka.

Desemba 31 mwaka huohuo, mabomu matatu yalilipuka mfululizo, mawili katika treni ya mwendo kasi (TGV au Train a Grande Vitesse) na jingine katika Kituo kikuu cha reli na mabasi cha mji wa Marseille nchini Ufaransa, ambayo yaliua watu watano.

Treni ya TGV ilikuwa imebeba abiria na ilikuwa inaelekea Paris na mabomu hayo yalilipuka wakati ikiwa njiani kusini mwa mji wa Lyon. Ndani ya treni hiyo abiria watatu waliuawa na wengine zaidi ya 30 walijeruhiwa na mlipuko huo.

Milipuko hiyo ililaribu kabisa behewa namba tatu la abiria ambalo lilipasuka vipandevipande. Mabaki ya behewa hilo yalikutwa juu ya paa za nyumba zilizokuwa mita kadhaa mbali na reli.

Katika kesi hii iliyohusu ulipuaji wa mabomu hayo, Carlos alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kingine cha maisha.

Hata hivyo, alikata rufaa na rufaa dhidi ya hukumu hiyo ikaanza Mei 2013. Carlos alishindwa rufaa hiyo.

Katika hukumu iliyotolewa na majaji Jumatano ya Juni 26, 2013 katika mahakama maalumu ya kupambana na ugaidi, ilisisitiza Carlos aendelee kutumikia kifungo cha maisha.

Jumanne ya Oktoba 7, 2014 Carlos alifunguliwa mashtaka mengine mapya kwa shambulio la bomu alilolifanya kwenye duka la dawa mjini Paris Jumapili ya Septemba 15, 1974 ambako watu wawili waliuawa na 34 kujeruhiwa.

Baada ya jitihada nyingi za wanasheria wake kupinga kusikilizwa kwa kesi hiyo huku wakijitahidi kumnasua kwa njia ya rufaa dhidi ya hukumu zilizomtia hatiani na kupewa hukumu ya vifungo vya maisha, hatimaye Mei 2016 mahakama iliamua kesi hiyo pia isikilizwe.

Kesi hiyo ilichukua muda mrefu kuanza kusikilizwa kwa sababu awali ilifutwa kwa kukosa ushahidi kabla ya kufunguliwa tena. Mawakili wake walidai mafaili yaliyotumwa polisi wa Ujerumani Mashariki yalikuwa na ushahidi usioaminika.

Kesi ilisikilizwa kwa siku chache kuanzia mwanzoni mwa Machi 2017. Hukumu ilitolewa Machi 28, 2017. Safari hii alihukumiwa kifungo kingine cha tatu cha maisha.

Machi 5, 2018 Carlos akiwa na umri wa miaka 68, mawakili wake walikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ya 2017 lakini akaangukia pua, Mahakama ya Rufaa ya Ufaransa ilisisitiza aendelee kutumikia iliyotolewa Machi 2018 na Mahakama Kuu ya nchi hiyo.

Majaji watano waliona Carlos alikuwa na hatia ya kutupa guruneti ndani ya uwanja, na kuua watu wawili na kujeruhi 32. Mara ya mwisho Carlos kuonekana mahakamani ni Jumatatu ya Machi 5, 2018 wakati alipokwenda kukata rufaa dhidi ya hukumu ya tatu ya kifungo cha maisha aliyohukumiwa Machi 2017.

Francis Vuillemin, ambaye alikuwa rafiki wa muda mrefu wa Carlos, pamoja na Isabelle Coutant-Peyre, ambaye kwa wakati huu alikuwa mshirika wake, walisema wanapambana ili aachiwe huru.

Ingawa alitamani sana kuwakomboa Wapalestina, njia aliyoitumia ilimfikisha gerezani badala ya kwenye ukombozi aliowazia.

Mambo mengi aliyopanga hayakufanikiwa malengo yake. Sehemu ya mipango mingi iliyoshindwa ni pamoja na lile jaribio la nchini Uingereza la kumuua Joseph Edward Sieff hata baada ya kumfyatulia risasi na kushindwa kuwaua mawaziri wa nchi za OPEC pamoja na kwamba aliwaweka mateka kwa siku kadhaa kabla ya kuwaachia.

Ni kwa sababu ya watu kama Carlos ndiyo maana mataifa mengi yamelazimika kuweka ulinzi mkali katika viwanja vya ndege, majengo ya Serikali pamoja na kwenye balozi mbalimbali.

Kwa ujumla Carlos anahusika na vifo vya watu 28 na kuwasababishia wengine 257 majeraha na vilema. Vyanzo vingine, kama gazeti ‘The Washington Post’ la Agosti 16, 1994 vinasema alisababisha vifo vya watu 83.

Hadi sasa, Carlos yuko gerezani kwa zaidi ya miaka 20 tangu alipokamatwa Agosti 1994 nchini Sudan.

Kama ataendelea kuwa hai, Oktoba mwaka huu wa 2021 atatimiza umri wa miaka 72. Je, kuna tumaini la yeye kuachiwa huru wakati wowote? Huenda halipo, lakini bado mawakili wake wanazungumza kuhusu ‘ufumbuzi’ wa suala la yeye kuachiwa huru.

Kwa mujibu wa simulizi fulani fulani, hofu kubwa aliyonayo ni kwamba mwisho wake hautakuwa mzuri. Mbali na kutumia sehemu kubwa ya maisha yake akiwa gerezani, anayo hofu ya kuuawa kwa sumu.

Mwandishi John Follain alimnukuu Carlos akisema: “Nitakaa gerezani milele au nikitoka nje nitapigwa risasi na kufa. Sitatoka Ufaransa nikiwa hai.”

Wakati mmoja kabla ya kukamatwa, alimwambia rafiki yake mmoja: “Sikiliza bwana, napenda maisha. Napenda kuyafurahia maisha kwa sababu sijui ni lini nitauawa. Najua kwamba siku moja nitauawa. Ndiyo maana unaona napenda sana maisha.”

Iwe anapenda sana kuishi au la, matendo yake yalisababisha vifo vya watu 28 na kujeruhi wengine 257. Mwisho wa matendo hayo ulijulikana Agosti 15, 1994, lakini mwisho wa maisha yake haujulikani.

Kesho tutasoma maisha ya Carlos gerezani.