Carlos atupwa Gereza La Sante -18

Carlos atupwa Gereza La Sante -18

Muktasari:

  • Katika matoleo yaliyopita tuliona maisha ya Carlos the Jackal akiwa uraiani hadi pale alipokamatwa nchini Sudan na kupelekwa Ufaransa kukabiliana na mashtaka yaliyohitimishwa kwa kuhukumiwa kifungo cha maisha.

Jaji Yves Corneloup alimkuta Carlos na hatia na kufungwa kifungo cha maisha wakati akiwa na umri wa miaka 48.

Lakini kulikuwa na kesi nyingine dhidi yake katika nchi nyingine ambazo zilimsubiri kuzijibu pamoja na kwamba tayari alikuwa amehukumiwa adhabu hiyo.

Carlos atupwa Gereza La Sante -18

Hukumu ya kwanza ilikuwa Jumatano, Desemba 24, 1997 alipopatikana na hatia ya mauaji aliyoyafanya Ufaransa Ijumaa ya Juni 27, 1975 nchini humo.

Hukumu ya pili ya kifungo cha maisha iliyotolewa na jopo la majaji watatu iliyotolewa Jumatano ya Juni 26, 2013 na hukumu ya tatu ilikuwa Jumanne ya Machi 28, 2017, wakati huu akiwa na umri wa miaka 67.

Hukumu ya Machi 2017 ilitokana na kesi iliyohusu kitendo chake cha kurusha bomu la kutupwa kwa mkono kwenye duka moja jijini Paris na kuua watu wawili na wengine 34 kujeruhiwa vibaya.

Aliiita hukumu hiyo ni “upuuzi”, akidai kuwa kitendo hicho alichokifanya miaka 43 iliyokuwa imepita, yaani mwaka 1974, kilikuwa ni cha kishujaa kwa sababu kilitekelezwa kwa jina la “mapinduzi” na akawalaani mawakili aliowataja kama ni “matapeli” na mawakala wanaosimamia “masilahi ya Wayahudi.” Tukio hilo alilifanya Jumapili, Septemba 15, 1974.

“Hakuna mtu aliyeua watu wengi kuliko mimi katika harakati za Wapalestina,” aliiambia mahakama hiyo na kuongeza, “mpaka sasa ni mimi pekee nimesalimika na niko hapa.”

Katika mapambano yote, kulikuwa na waathiriwa, ni bahati mbaya sana hali ilikuwa hivyo.” Habari hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Machi 28, 2017. Msumari wa mwisho ulipigwa na Mwendesha Mashtaka wa Ufaransa, Remi Crosson du Cormier, ambaye aliiomba Mahakama imhukumu Carlos kifungo cha maisha, kwa jina la sheria na kwa ajili ya walioathirika bila kujali kama anatumikia vifungo vingine vya maisha katika gereza la Ufaransa.

Jopo la majaji watano lililokuwa likiisikiliza kesi hiyo likiongozwa na Jaji Francois Sottet halikusita kutoa hukumu hiyo.

Kesi hiyo ambayo ilisikilizwa kwa wiki mbili mfululizo, Carlos aliiambia mahakama hapaswi kulazimishwa kutoa ushahidi dhidi yake mwenyewe. Ingawa alikana mara kwa mara kuhusika na shambulio hilo la duka la dawa jijini Paris, kuna wakati aliwachekesha waendesha mashtaka aliposema; “Labda ni mimi, lakini hakuna uthibitisho wowote. Sina hatia, lakini kwa mtazamo wangu kesi hii yote ni upuuzi.”

Kutokana na hukumu hiyo, sasa Carlos akawa na uhakika kuwa hatatoka tena gerezani hata siku ya mwisho ya maisha yake duniani. Alichukuliwa na kupelekwa kwenye Gereza la La Sante ambako alichukuliwa tena alama za vidole, akapekuliwa, akakabidhiwa shuka na blanketi jingine, vifaa vya malazi ambavyo aliviweka kwapani na kwenda garezani akiwa miongoni mwa wafungwa wanaolindwa zaidi.

Wafungwa wengine ambao wamewahi kulindwa sana katika historia ya gereza hilo ni Guillaume Apollinaire (mwaka 1911) na Henri Landru (mwaka 1919), lakini hawakuwa magaidi kama Carlos.

Apollinaire alikuwa malenga wa Ufaransa, alifungwa kwenye gereza hilo kwa wizi wa kazi za watu.

Kitabu ‘A French Song Companion’ kilichoandikwa mwaka 2000 na waandishi wawili, Graham Johnson na Richard Stokes, kinasema Apollinaire aliingia matatani kwa tuhuma za kuiba kazi za watu za uandishi, akatunga nyimbo na kujifanya mashairi aliyotumia ni yake. Kwa upande wa Guillaume Apollinaire, yeye alikuwa ni mshairi Mfaransa, mwandishi wa riwaya, historia inamchukulia kama mmoja wa washairi mashuhuri zaidi wa mwanzoni mwa karne ya 20.

Lakini pia aliponzwa na kashfa ya wizi wa kazi za watu. Alikamatwa na kushtakiwa, kisha Septemba 7, 1911 akahukumiwa kifungo katika gereza hilo na kupewa ulinzi mkali.

Mfungwa mwingine aliyelindwa zaidi katika historia ya gereza hilo ni Henri Landru (1869–1922) ambaye alifungwa kwa kosa la kufanya mauaji ya mfululizo nchini Ufaransa.

Landru ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Bluebeard of Gambais, kwa nyakati tofauti aliua wanawake wasiopungua saba katika kijiji cha Gambais kati ya Desemba 1915 na Januari 1919.

Mwandishi Mitzi Szereto katika kitabu chake, ‘The Best New True Crime Stories: Serial Killers’ anasimulia kuwa Landru pia aliwaua wanawake wengine wasiopungua watatu, pamoja na kijana mmoja katika nyumba aliyoikodi tangu Desemba 1914 hadi Agosti 1915 katika mji wa Vernouillet, kilometa 35 Kaskazini Magharibi mwa Paris.

Hata hivyo, mwandishi mwingine, Maria Tatar katika ukurasa wa 135 wa kitabu chake cha ‘Secrets Beyond the Door: The Story of Bluebeard and His Wives’, ameandika hivi: “Idadi ya kweli ya waliouawa na Landru ambao mabaki ya miili yao hayakupatikana kamwe ni kubwa zaidi na haitajulikana kamwe.”

Inaelekea Landru alikuwa mkatili sana kwa wakati wake. Simulizi nyingine zinazomhusu, kama iliyoko kwenye kitabu cha ‘World Serial Killers: They Kill for the Thrill’ cha Gordon Kerr kinasema, Landru alikuwa akiwarubuni wanawake kwamba atawaoa, hususan wanajeshi walioshiriki katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Kisha alikuwa akifanya nao ngono baadaye anawaua kwa kuwakatakata miili yao. Hivyo katika historia ya Gereza la La Sante lenye umri wa miaka 154, limekuwa na wafungwa watatu tu katika historia hiyo ambao wamelindwa zaidi kuliko mfungwa mwingine yeyote katika historia ya gereza hilo inayozidi karne moja na nusu.

Kwa muda mrefu, kwa mujibu wa wanahistoria, imejulikana kuwa Gereza la La Sante limekuwa na sifa mbaya kwa muda fulani wa historia ya kuwapo kwake kuliko magereza mengine ya nchi hiyo.

Hilo ndilo gereza ambao Carlos hakuwazia kuwa angekuwa mfungwa ndani yake. Hata hivyo, baadhi ya wafungwa walifanikiwa kutoroka katika gereza hilo katika nyakati fulani.

Wiki moja kabla Carlos hajawasili kwenye gereza hilo, mfungwa mmoja ambaye alifungwa kwa sababu ya ubakaji alifanikiwa kutoroka kwa kukata chuma cha mahabusu. Haikujulikana alivyopata msumeno.

Miaka minane kabla, jambazi aliyeitwa Michel Vaujour alitoroshwa kwa kuchukuliwa na mkewe, Nadine, kwa helikopta juu ya paa la gereza, na mwaka 1978 jambazi mwingine, ambaye alikuwa adui mkubwa wa umma, Jacques Mesrine, alimpora mlinzi wa gereza sare zake, bunduki na gesi ya kutoa machozi na kuvitumia kutoroka.

Carlos aliwahi kuwaza kutoroka gerezani? Tukutane kesho.