Carlos mjanja alivyonasa kwenye tundu bovu -15

Carlos mjanja alivyonasa kwenye tundu bovu -15

Muktasari:

  • Wiki mbili baada ya Rais wa Iraq, Saddam Hussein kuamuru vifaru vyake kuivamia Kuwait Agosti 2, 1990, mashirika mengi ya kijasusi ya nchi za Magharibi yalianza kufuatilia nyendo za Carlos baada ya kunasa taarifa kwamba Saddam alikuwa tayari kumtumia kushambulia maslahi yao.

Wiki mbili baada ya Rais wa Iraq, Saddam Hussein kuamuru vifaru vyake kuivamia Kuwait Agosti 2, 1990, mashirika mengi ya kijasusi ya nchi za Magharibi yalianza kufuatilia nyendo za Carlos baada ya kunasa taarifa kwamba Saddam alikuwa tayari kumtumia kushambulia maslahi yao.

Lakini wakati huo, Carlos hakuwa Iraq bali Damascus, Syria, nchi ambayo haikukubaliana na uvamizi wa Iraq nchini Kuwait.

Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) liliwasukuma majasusi wa Ufaransa (DST) katika jaribio la kumkamata Carlos.

Wakati wanajeshi karibu 500,000 wa Marekani na washirika wake wakijikusanya Saudi Arabia kujiandaa kupambana na Iraq, majasusi wa Syria waliwasaidia CIA na DST njia za kificho za kumkamata Carlos.

Ili wasionekane wamemsaliti mgeni wao kwa CIA na DST kwa kumnyakua Carlos Syria, ilipangwa asafiri kwenda nchi nyingine ambako angekamatwa.

Starehe alizopewa na Rais Hafez al-Assad zilipopungua kwa kuminywa vyanzo vya fedha, mwaka 1990 aliamua kutembelea Hungary na Czechoslovakia kuchukua fedha zilizosalia kwenye akaunti zake nyingi za benki.

Licha ya mpango wa safari kuwafikia CIA na DST, Carlos aliahirisha safari kutokana na wasiwasi kuwa vita vya Ghuba vingemzuia ashindwe kurejea Syria.

Akiwa bado Syria, watu wake wa karibu walianza kumwona kama mzigo. Desemba 1991 Syria ilimwondosha Carlos na mkewe, Magdalena kwenda Yemeni.

Ubalozi wa Yemeni ulimpatia pasipoti kwa jina la Abdurabo Ali Mohamed. Yeye na familia yake walikwenda Jordan mwishoni mwa 1991 bila majasusi wa nchi za Magharibi kujua.

Katikati ya mwaka 1992 ndipo majasusi wa Jordani wakagundua uwapo wake nchini humo. Ingawa alipewa hifadhi ya miezi michache, ilipogundulika kuwa alimuua ofisa wa Serikali ya Iraq nchini Austria, hakuruhusiwa tena kuendelea kubaki nchini Jordan.

Aliwapakia mkewe, mama yake na binti yake kwenda Venezuela, na yeye aliondoka kwenda Cyprus.

Kabla ya kuondoka Jordan alikuwa ameoa mke wa pili, Abdel Salam Adhman Jarrar Lana. Baadaye aliwasiliana na watu wake katika Serikali ya Iran, lakini walikataa kumpokea ingawa walimpa dola milioni 1.2 na kumshauri aende kuishi Sudan.

Baada ya kuona hana pengine pa kwenda, yeye na Lana walielekea Sudan Oktoba 1993 wakiongozana na gaidi aliyeitwa Ali Al Issawe (Abu Hakam) ambaye awali alikuwa ofisa wa polisi wa siri wa Syria. Sudan walimpokea.

Akiwa Khartoum alijiita Dk Abdallah Barakhat na kwamba alikuwa raia na mfanyabiashara wa Jordan.

Yeye na mkewe walijichanganya na watu na hata kwenda vilabu vya usiku na kwenye mialiko ya sherehe wakiwa na walinzi binafsi.

CIA na DST hawakuacha kufuatilia nyendo zake. Ndani ya wiki kadhaa baada ya Carlos kuwasili Sudan, makachero wa Syria waliiambia CIA kwamba yupo Khartoum.

Kitengo cha CIA kinachokusanya taarifa za kijasusi za nchi za kigeni kilituma timu ya majasusi wenye asili ya Afrika kwenda Khartoum. Walikaa kwa wiki kadhaa wakimfuatilia, walifanikiwa kukaa na kunywa naye bila yeye kuwatambua.

Baada ya kupata naye kinywaji katika Klabu ya Armenia katikati ya Khartoum, mmoja wa majasusi hao alifanikiwa kuichukua glasi tupu aliyotumia Carlos wakati amempa kisogo.

Alama za vidole katika glasi hiyo zilitumwa CIA kufanyiwa uchambuzi wa kina kuthibitisha kuwa huyo wanayemfuatilia ni Carlos.

Huo ndiyo ukawa wakati wa kuwaambia Wafaransa kuwa huyo waliyekuwa wanakunywa naye ndiye Carlos na wala si Dk Abdallah Barakhat. Baada ya kuthibitishiwa, Wafaransa walipata nafasi ya kujenga uhusiano ‘mzuri’ zaidi na Sudan.

Wakati hayo yakiendelea, baadaye, Carlos alilazimika kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mafuta kwenye kiuno chake. Upasuaji huo ulipangwa kufanyika katika Hospitali ya Ibn Khaldoun mjini Khartoum na ulifanyika jioni ya Jumamosi, Agosti 13, 1994.

Kwa muda wote aliokuwa hospitalini aliruhusiwa na Serikali ya Sudan kuweka walinzi wake hata kwenye korido za hospitali nje ya chumba alicholazwa, na siku moja kabla ya kufanyika kwa upasuaji huo mkewe Lana naye aliruhusiwa kulala hospitalini hapo.

Alipotolewa chumba cha upasuaji alirejeshwa chumbani kwake na kuangaliwa na Lana. Kabla hajazinduka sawasawa alipata mgeni aliyejitambulisha kuwa ni ofisa wa Serikali ya Sudan kutoka idara ya upelelezi wa makosa ya jinai.

Ofisa huyo alimweleza Carlos kwamba polisi wa Sudani wamegundua kuna njama za kumuua. Alimsihi akubali kuhamishwa kutoka hospitali hiyo na kupelekwa hospitali ya jeshi ambako usalama wake ungekuwa mkubwa zaidi.

Ingawa hakumwamini ofisa huyo, hakumkatalia. Wakati anatolewa, watu wenye silaha walimsubiri nje ya hospitali hiyo. Badala ya kupelekwa hospitali ya jeshi kama ilivyoelezwa awali, Carlos na Lana walipelekwa Makao Makuu ya Usalama ya Sudan.

Kutoka hapo mpango ulibadilishwa. Kwa ridhaa ya Carlos, msafara ulielekea nje kidogo ya jiji la Khartoum na kuwekwa katika nyumba moja katika shamba, yenye bustani kubwa.

Siku iliyofuata, Jumapili ya Agosti 14, Carlos na Lana walitamani sana kurudi nyumbani kwao walikokuwa wamefikia, lakini haikuwezekana kutokana na ulinzi mkali uliokuwapo. Daktari aliyeletwa kuangalia maendeleo ya afya ya Carlos hakujibu swali lolote aliloulizwa na Carlos.

Carlos na Lana wakalazimika kulala usiku wa pili kwenye nyumba hiyo ambayo hawakuipenda. Saa nne usiku Carlos alimtuma mkewe na dereva wake kwenda kuchukua vitu kadhaa katika nyumba waliyokuwamo kabla.

Lana alipokawia kurudi, Carlos hakuendelea kumsubiri kwa sababu usingizi ulimchukua, akalala. Saa tisa usiku alihisi akipumua kwa shida na mapafu yamebana na kuhisi viungo vyake vimebana kwenye godoro.

Alizinduka kitandani akitaka kukimbilia bastola yake kando ya kitanda, lakini hakupata nafasi hiyo. Aliwaona walinzi wake wa Kisudan wakiwa miongoni mwa watu zaidi ya 10 waliojazana kwenye chumba alicholala.

Ndipo akagundua kuwa mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa pingu kwa nyuma.

Akiwa hajajua vyema kilichotokea, alikuja daktari wa Jeshi la Sudan, akamwendea Carlos, akamshika na kumchoma sindano kwenye paja. Kwa muda mfupi Carlos aliamini ilikuwa ni sindano ya sumu, lakini mmoja wa waliokuwa kwenye chumba hicho alimwambia hiyo ni sindano ya kumtuliza.

Kidogo kidogo Carlos akaanza kusinzia na baadaye fahamu zikatoweka moja kwa moja. Ndipo walipombeba, wakamtoa ndani ya chumba hicho na kumpeleka katika gari iliyokuwa ikisubiri nje ya nyumba hiyo. Alifungwa mikono na miguu, akawekwa kwenye machela na kuingizwa kwenye gari.

Je, baada ya kumkamata Carlos walimpeleka wapi?

Tukutane toleo lijalo.