CCM, Chadema vyawalilia waliofariki kwa mafuriko Hanang

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vimetoa salamu za pole kufuatia vifo vilivyosababishwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha mkoani Manyara.

Dar es Salaam. Baada ya taarifa ya vifo vilivyosababishwa na mafuriko ya tope katika eneo la Katesh na Gendabi wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vimetuma salamu za rambirambi kufuatia vifo hivyo.

CCM imetoa pole kwa wananchi wa Wilaya ya Hanang kufuatia mafuriko yanayoendelea hadi sasa ambayo yamesababisha vifo vya watu 20 na majeruhi na uharibifu mkubwa wa miundombinu, ikiwemo mashamba na makazi ya wananchi.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda imesema  Chama kinawapa pole wote walioguswa na vifo hivyo kwa namna moja au nyingine, wakiwemo waliopoteza wapendwa wao, ndugu, jamaa, marafiki.

“Tunawatakia uponaji wa haraka majeruhi wote wa mafuriko hayo wanapoendelea kupata matibabu. Chama kinatoa wito kwa wananchi waendelee kuchukua tahadhali na kuitaka serikali na vyombo vinavyohusika na uokoaji viendelee na jitahada za uokoaji,” ameeleza Makonda kupitia taarifa hiyo.

Kwa upande wa Chadema kupitia taarufa yake iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema mbali ya kuguswa na vifo hivyo wametoa wito kwa Serikali kuhakikisha inaimarisha mifumo ya utambuzi wa mapema wa majanga nchini ili kuweza kutoa tahadhari kwa wananchi kabla majanga hayajasababisha maafa makubwa kama haya.

“Chaema kimepokea kwa majonzi, simanzi na huzuni kubwa taarifa za vifo vya watanzania 20 vilivyotokea Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara, vilivyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kuonyesha nchini,” amesema Mrema

Aidha, chama kimetoa salamu za pole na rambirambi kwa ndugu, jamaa, marafiki na watanzania wote kwa msiba huu mkubwa. Pia kinawaombea majeruhi wapone haraka warejee katika siha njema.

“Tunawahimiza viongozi na wanachama wetu mkoani Manyara kutoa msaada kwa kadiri ya uwezo wao kwa wahanga wote katika kipindi hiki kigumu,” amesema Mrema

Pia, Chama kimeitaka Serikali kutoa bajeti ya kutosha kwenye mfuko wa Taifa wa maafa ili uweze kununua vifaa vya kisasa vya uokoaji pindi maafa yanapotokea popote pale nchini.

“Tunasisitiza ushauri wetu wa kisera wa kulifanya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa sehemu ya halmashauri ili kila halmashauri iweze kujihudumia na kuwa karibu zaidi na wananchi na kuweza kutoa huduma za dharura pindi maafa yanapotokea.”

Hadi leo Jumapili mchana wa Desemba 3, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja akizungumza na Mwananchi Digital, amesema hadi mchana (saa 7.30) miili 20 imepatikana na majeruhi 70 wanatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tumaini.

Akiwa Dubai alikohudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pia ametoa salamu za pole kwa wananchi walioathirika na mafuriko katika eneo hilo.

Aidha, Rais Samia ametoa maelekezo kwa vyombo vinavyoshughulikia maafa na wizara husika kufika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada.