CCM Simanjiro yaziba nafasi ya kiongozi aliye mahabusu

Monday September 13 2021
CCM pc

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya wazazi wa CCM Kata ya Endiamtu, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Ernest Lukumay akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua kwenye nafasi hiyo, kushoto ni Katibu wa CCM Kata ya Endiamtu, Anthony Mavili. Picha na Joseph Lyimo

By Joseph Lyimo

Mirerani. Wajumbe wa Halmashauri ya CCM Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamemchagua Ernest Lukumay kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wa Kata hiyo ili kuziba nafasi ya Kalinga Ally aliyepo mahabusu kwa tuhuma za kumuua mama yake.

Kwa miaka mitatu mfululizo nafasi ya Mwenyekiti wa wazazi wa kata hiyo ilikuwa wazi baada ya Kalinga kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwenye mahakama ya Mkoa wa Manyara Mjini Babati ya kumuua mama yake kwa kumchomea ndani ya nyumba.

Kutokana na hali hiyo nafasi hiyo iligombewa upya ambapo wajumbe watatu walichukua fomu na kuingia kwenye kinyanganyiro ambapo Lukumay akaibuka kidedea.

Katibu wa CCM kata ya Endiamtu, Antony Mavili amesema pia wajumbe hao walijaza nafasi ya Katibu wa wazazi wa kata hiyo baada ya Hamad Malya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kazamoyo.

Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa uchaguzi huo Rajabu Msuya amesema, Lukumay aliwashinda wapinzani wake wawili kwa kupata kura 14 kati ya wajumbe waliopiga kura 15.

Msuya amesema nafasi ya pili ilishikwa na Ally Juma aliyepata kura moja na nafasi ya tatu ilishikwa na Chacha Ngogo aliyetoka patupu kwa kukosa kura.

Advertisement

Msuya amemtangaza mshindi wa nafasi ya Katibu kuwa ni Agripina Paulo aliyepata kura 10 kati ya kura 15 zilizopigwa huku nafasi ya pili ikienda kwa Daniel Philbert Ndaikya aliyepata kura nne na kura moja ikiharibika.

"Nachukua fursa hii nikiwa Mwenyekiti wa uchaguzi kuwashukuru wajumbe wote kwa kuhudhuria katika uchaguzi huu, kwani bila ya ninyi uongozi huu tulioupata tusingeupata, pili niwapongeze wajumbe kwa kupata uongozi mpya," amesema Msuya.

Msimamizi wa uchaguzi huo Katibu wa Kata ya Endiamtu Antony Mavili amewataka viongozi hao wapya kufanya kazi kwa weledi ili kuweza kuifufua jumuiya hiyo ya Wazazi ambayo ilionekana kama ilikufa katika kata hiyo.

"Kuwepo kwanu sasa ni wajibu wanu kuhakikisha mnachapa kazi ili kuleta matumaini mapya kwa wajumbe waliowaweka madarakani lakini kubwa kumsaidia Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi," amesema Mavili.

Mwenyekiti mpya wa wazazi kata ya Endiamtu Ernest Lukumay amewashukuru wajumbe kwa kumuweka madarakani huku akiahidi kutoa ushirikiano wa dhati ili kuweza kutekeleza majukumu husika.

"Hakika leo siku yangu imefika, wakati najinadi hapa mbele yenu moyoni mwangu nikawa nasema Mungu usiniaibishe, uwezo wa kuwatumikia ninao, ninachohitaji leo kwa Mungu ni kupata kibali chako tu cha kupata hii nafasi, Mungu sifa na utukufu ni kwako, hakika wewe ni Mungu usiyeshindwa milele na milele," amesema Lukumay.

Advertisement