CCM waanza kufanya kazi kwa zamu

CCM waanza kufanya kazi kwa zamu

Muktasari:

Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM,   Humphrey Polepole amesema chama hicho kimeanza kufanya kazi usiku na mchana kutatua kero za wananchi.

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM,   Humphrey Polepole amesema chama hicho kimeanza kufanya kazi usiku na mchana kutatua kero za wananchi.

Polepole amesema hayo leo Ijumaa Novemba 20, 2020 wakati akizungumza na waandashi wa habari  kuhusu yaliyojiri katika kikao cha kamati kuu ya chama hicho kilichoketi jana.

Amesema pamoja na ajenda mbalimbali zilizojadiliwa katika kikao hicho kilichoongozwa  na  mwenyekiti wa chama hicho,John Magufuli.

Kikao  hicho kilithibitisha majina ya uteuzi wa wagombea wa umeya wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya.

Kabla ya kutangaza majina ya wanachama waliopitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho, Polepole aliwatahadharisha walioteuliwa akisema kipindi hiki chama hakitawavumilia viongozi wazembe.

 “Hatuna muda wa kupoteza, kipindi hiki CCM nimeshawaeleza kuwa kabla na wakati wa  uchaguzi mkuu tunafanya kazi kwa ‘shift’, wako watu wanaofanya kazi mchana na wako watu wawanaofanya usiku na kuendelea kushughulikia na utatuzi wa kero za watu wetu, " amesema Polepole

Amesema nafasi zinazowaniwa Tanzania Bara ni; umeya katika majiji sita, manispaa nafasi 20, halmashauri za miji nafasi 22 huku nafasi 137 zikiwa ni za  uenyeviti wa halmashauri katika wilaya 137.

Amesema kuwa tofauti na vipindi vya nyuma ambapo uteuzi ulikuwa unaishia kwenye ngazi za chama za mkoa, kipindi hiki kamati kuu iliamua uteuzi uidhinishwe na kamati kuu.

“Chama cha Mapinduzi kipindi hiki tunapenda kufanya kidogo tofauti, Ni desturi mwanzoni huko viongozi hawa wa halmashauri kote nchini Tanzania walikuwa wanapitishwa na ngazi ya mkoa ya chama lakini Kamati Kuu imependekeza kipindi hiki viongozi wetu wa halmashauri zote ni lazima kamati kuu ya halmashauri kuu ya taifa iwathibitishe” amesema

Amesema kuwa sababu ya wagombea hao kuithibitishwa na Kamati Kuu ni kutokana na uhitaji wa kupata viongozi ambao wanaendana na kasi ya Rais John Magufuli.