CCM yajipanga kulipa posho mabalozi wa mashina Zanzibar

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema umefika wakati chama hicho kuwalipa posho mabalazi wa mashina.

Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema umefika wakati chama hicho kuwalipa posho mabalazi wa mashina.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Mei 4, 2023 wakati akizungumza na viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya mashina hadi Mkoa wa Kusini Unguja na kutembelea miradi ya chama hicho.

Amesema watendaji hao wanajitolea kwa muda mrefu ndani ya chama hicho lakini hawapati chochote.

Amemuagiza Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Dk Muhammed Dimwa kuandaa utaratibu wapatiwe vitambulisho maalumu waanze kulipwa posho

"Wakati umefika sasa tuwape posho mabalozi hawa kwasababu wanafanya kazi kubwa. Natoa maagizo sasa andaa utaratibu wawe na vitambulisho maalumu," amesema

Amesema kumekuwepo na ugumu wa chama hicho kuwalipa mabalozi hao kwasababu ya wingi wao maana wapo zaidi ya 5,000.

Akizungumzia kuhusu uimara wa chama, amewataka kuvunja makundi na kuwa wamoja ili wajenge chama chao kusafisha njia ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Amesema chama hicho kina miradi mikubwa ambayo inaweza kukiwezesha kukijenga na kuwa na uchumi imara.