CCM yathibitisha majina wagombea umeya, uwenyekiti

CCM waanza kufanya kazi kwa zamu

Muktasari:

Chama cha Mapunduzi (CCM) kimepitisha majina kadhaa ya wagombea umeya wa majiji, manispaa na uwenyekiti wa halmashauri za wilaya na miji.

Dar es Salaam. Chama cha Mapunduzi (CCM) kimepitisha majina kadhaa ya wagombea umeya wa majiji, manispaa na uwenyekiti wa halmashauri za wilaya na miji.

Kabla ya kufikia uamuzi huo, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho chini ya mwenyekiti wake,   John Magufuli ameagiza kufanya mapitio na mchujo wa wagombea wote wa nafasi hizo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema baada ya kikao cha kamati kuu kilichofanyika jana  kuchambua majina yote ya wagombea imethibitisha jina la mgombea mmoja kati ya saba walioomba nafasi ya umeya wa Jiji la Dodoma.

“Zamani mchakato wa kuwapata viongozi hawa ulifanyika ngazi ya mkoa sasa kamati kuu ikapendekeza halmashauri zote iwathibitishe kabla ya kupigiwa kura na baraza la madiwani,” amesema Polepole.

Katika majiji mengine matano, Kamati imethibitisha wagombea watatu kati ya tisa (Dar es Salaam), watatu kati saba (Mwanza),watatu kati ya 10(Mbeya), watatu kati ya 17(Arusha), watatu kati ya sita(Tanga).

Polepole amesema kamati ilipokea majina ya wagombea 150 wanaowania umeya kwenye halmashauri 20 za manispaa, majina 137 wanaowania uwenyekiti katika halmashauri 137 za wilaya na majina 109 wanaowania uenyekiti katika halmashauri 22 za miji.

Kabla ya kutaja orodha ya majina ya wagombea wanaotakiwa kuanza kupigiwa kura Novemba 23 na 24, 2020 Polepole amesema kamati imefikia uamuzi huo ili kupata viongozi waadilifu, wazalendo na wachapa kazi zaidi.

Polepole amesema kamati kuu imethibitisha jina la mgombea mmoja tu katika nafasi za umeya wa manispaa na halmashauri za miji na wilaya kadhaa huku ikiagiza mchakato urudiwe kwenye halmashauri saba za miji na wilaya.

Amesema kamati imeagiza marudio ya mchakato wa kupata wagombea uanze mara moja kwa halmashauri zilizotakiwa kurudia upya ikiwa ni lengo la kupanua wigo wa demokrasia.