CCM yatoa onyo watendaji wazembe serikalini

New Content Item (1)

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akizungumza na wanachama wa chama hicho Dodoma

Muktasari:

  • Watendaji ndani ya CCM na Serikali wametakiwa kukaa mguu sawa katika utendaji kwani chama hicho kimesema hakitamvumilia mtu yeyote anayekwenda kinyume na matakwa ya watu.

Dodoma. Watendaji ndani ya CCM na Serikali wametakiwa kukaa mguu sawa kwani chama hicho hakitamvumilia mtu anayekwenda kinyume na matakwa ya watu.

Rai hiyo imetolewa leo Jumanne Januari 24, 2023 na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo wakati akitoa salamu za chama kwenye mapokezi ya Sekretarieti mpya ya chama hicho jijini Dodoma.
Amesema kilichoifikisha Tanzania mahali ilipo sasa ni suala la kuchekeana chekeana hivyo huu si wakati wa kuangaliana bali ni kutenda zaidi kwa ajili ya wananchi.
Chongolo amesema Taifa limejaa walalamikaji kila wakati na hata ambao wana mamlaka ya kutokulalamika nao wanalalamika kitu kinachoshangaza.
Kutokana na hilo amesema huu si wakati wa kupokea maneno tena badala yake wanataka wachapa kazi ambao wanaweza kukisaidia CCM kwenda mbele huku akionya atakayesababisha malalamiko.
Katibu mkuu wa chama amesema bila kutimiza wajibu na kama hali hiyo itaendelea Watanzania watakinyooshea kidole CCM jambo ambalo halitakubalika kwa mtu au watu kusababisha hayo yatokee.
“Sisi ndiyo tulioshika dola, hatutafuti dola bali tunatafuta kuilinda dola, sasa unakuta mtu mliyempa dhamana ya kuwasaidieni anafanya kazi kwa kulalamika tena anawalalamikia anaowaongoza, halikubariki hili,” amesema Chongolo.
Bila kutaja majina, lakini amesema kuna baadhi ya wateule katika nafasi za uwaziri nao hufika mbele ya vyombo vya habari na kuanza kulalamika hivyo wanasababisha na watendaji hata wa ngazi ya chini wanakuwa walalamishi.
Amesema kuanza sasa kundi la namna hiyo halitavumiliwa na hakutakuwa na msalia mtume kama mtu hatimizi wajibu wake aliokabidhiwa.
Katika hatua nyingine amesema wiki hii ataanza ziara katika mkoa wa Morogoro yeye na timu yake ambako huko watasikiliza kero za watu na kupata maelezo ya watendaji namna gani wanatatua kero hizo kwani hicho ndiyo kipimo kwa mtumishi wa Serikali na chama.