CCM yawataka wanaowania ubunge Mbeya Mjini wajipime

Baadhi ya Wananchi waliojitokeza kupata kadi ya bima zinazotolewa na Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson kwa kaya zaidi 300 kwa jiji la Mbeya. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya, Humphrey Msomba amewataka makada wa chama hicho wanaotaka kuwania ubunge katika jimbo la Mbeya Mjini kujitathimini kwanza.

Mbeya. Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbeya kimewataka makada wa chama hicho wanaotaka kuwania ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini kujitathmini, kwani chama hicho hakitaki kurejea kwenye kipindi kilichopita walipolipoteza jimbo hilo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Humphrey Msomba amesema leo Jumanne Januari 24, 2023 wakati Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kadi za  Bima ya  Afya ya Jamii iliyoboreshwa (ICHF)  kwa wazee, wajane na wasiojiweza 3,000 katika kaya 500  kupitia program ya Tulia Heath.
Msomba amesema kuwa tangu Spika Tulia awe Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, amekisaidia chama kutekeleza ilani yake ya uchaguzi kwa kuchangia katika sekta ya elimu, afya na miradi ya Maendeleo.
“Hatuko tayari kumpoteza Mbunge huyu kama viongozi tuko bega kwa bega kumlinda na kuhakikisha anaendelea kutekeleza ilani ya chama na kuwataka watakaokuja wasidhani yanayotamkwa ni nguvu ya soda,” amesema.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dour mohamed Issa amesema kama Madiwani hawako tayari kupoteza jimbo kwani kwa kipindi kifupi Jiji la Mbeya limepiga hatua kubwa katika nyanja za elimu, afya, barabara.
“Tunamlinda Spika wa Bunge na Mbunge Dk Tulia Ackson hatua kwa hatua usiku na mchana pia niwaonye wananchi kuachana na tabia ya kuwa chawa na kugunguni,” amesema.

Issa ameseme uwepo wa Spika Dk Tulia, amesaidia kuwaweka sawa na kuwaunganisha Madiwani wa Jiji la Mbeya kuwa wamoja na kusimamia miradi ya Maendeleo tofauti na miaka ya nyuma.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua amesema kuwa ni wakati sasa kwa  Wanambeya kutambua wana deni la kumlipa Dk Tulia, kwani kitendo cha kutoa bima kwa kata 3,000 sio jambo dogo.