CCT yaiangukia Serikali kutoza kodi huduma za elimu, afya

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk Fredrick Shoo (kushoto) ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya CCT iliyofanyika kitaifa katika Usharika wa Moshi mjini mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Kilio cha kodi kwa taasisi za dini ni kikubwa na endapo hilo halitaangaliwa, litasababisha baadhi ya taasisi kujifunga kwa kushindwa kujiendesha.

Moshi. Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imeiomba serikali kulitazama suala la kodi kwa taasisi za dini zinazotoa huduma za Afya na elimu, kwa kuwa linatishia uhai wa taasisi hizo.

Akzungumza Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk Fredrick Shoo amesema kilio cha kodi kwa taasisi hizo ni kikubwa na endapo hilo halitaangaliwa, litasababisha baadhi ya taasisi kujifunga kwa kushindwa kujiendesha.

Dk Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya CCT, ambapo yamefanyika kitaifa katika usharika wa Moshi mjini mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali, akiwemo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Amesema utozwaji wa kodi hizo lukuki ikiwemo za mapato na Ardhi zinafanya taasisi hizo kuonekana kama washindani au maadui kwa Serikali.

“Mambo ya kodi yanatuumiza sana taasisi za kanisa, yaani tunapigwa kodi nyingi tunafikia mahali ambapo tunaonekana washindani au kama maadui na nyingine zimefikia mahali ikiendelea hivyo itajifunga kutokana na kushindwa kujiendesha,” amesema Dk Shoo.

Ameongeza kuwa, “Leo Serikali kama imejiweza kujenga zahanati zake, vituo vya afya  na shule, ambapo najua bado haijatosha, lakini  isije ikawa ni sababu ya kupigana, yaani kuja na kodi hizi ambazo unajua kabisa kituo kikilipa hakika ni kama unataka kufunga kile kituo, naomba hekima itumike,” amesema.

“Nasema mambo haya hayapo sawa  waziri na hii haitakuwa baraka kwa nchi hii tukijua taasisi hizi, zinamuhudumia na zinasaidia katika kuongeza huduma kwa watanzania, kilio ni kikubwa, mkayafanyie kazi hili kwa baraka kwa manufaa ya nchi hii ya Tanzania,” amesema.

Aidha Dk Shoo ametumia pia nafasi hiyo kuiomba serikali,  kuendelea kulitazama suala la kodi kwenye taulo za kike (Sodo) ili kuwezesha upatikanaji wake kwa urahisi na kuondoa changamoto ambazo hupitia watoto wa kike wanapokuwa kwenye hedhi.

“Ndugu waziri najua kuna hatua zimechukuliwa na serikali katika suala hili la taulo za kike,  lakini naomba iendelee kuangalia jambo la kodi kwenye hili, Watoto wasije wakapata maambukizi kwa sababu ya kutumia matambara na vitu vingine  ambavyo havitunzi afya zao”

Dk Shoo amewataka pia wazazi na walezi kulitazama suala hilo, na kuhakikisha watoto wanapoomba fedha kwa ajil ya kununua taulo hizo wanahudumiwa, ili kuweza kuwa na hedhi salama.

Akitoa taarifa Katibu Mkuu wa CCT Dk Canon Matonya amesema jumuiya hiyo inafanya shughuli mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za serikali ambapo makanisa wanachama yanamiliki taasisi zinazotoa huduma za afya 219 na taasisi za elimu 255.

Amesema pamoja na jitihada hizo changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwapa ugumu katika kutoa huduma kwenye taasisi hizo ni kudaiwa kodi za mapato kutokana na huduma za afya na elimu wanazozitoa.

“Taasisi zetu nyingi za kanisa zinakabiliwa na changamoto ya kudaiwa kodi za mapato  kutokana na huduma za afya na elimu zinazotolewa,TRA wamekuwa na mtazamo kuwa taasisi hizi   zimekuwa zikiingiza faida kutokana na huduma hizo, tunaomba serikali itazame hili na kuondoa kodi hizo ili kuzisaidia taasisi kuendelea kutoa huduma".

Mbali na hilo, aliishauri serikali kufanya marekebisho ya sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu sekta binafsi  ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje katika shughuli za kilimo, viwanda na masoko.

“Tunaishauri serikali kuimarisha sekta binafsi kwa kuhamasisha watu kutoka ndani na nje ya nchi yetu kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha mashamba makubwa ya mazo ya chakula na biashara, lakini pia wawekezaji binafsi wahamasishwe zaidi kujenga viwanda vya kusindika mazao ya ndani ya nchi”

“ Serikali ifungue masoko ya uhakika ya wakulima wadogo wadogo, lakini pia tunashauri marekebisho ya sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu sekta binafsi yafanyike ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje katika shughuli za kilimo, viwanda na masoko”.

Akizungumza Waziri wa Fedha na mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema amepokea kwa niaba ya serikali maombi na ushauri uliotolewa na kwamba  suala la kodi kwa taasisi za dini, serikali imeendelea kulifanyia kazi  na itatoa taarifa  wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya mwaka 2023/2024.

“Niwaombe wote mkubali, kwa sababu kwa taratibu zetu za kikodi huwa hatutaji ni kipi tutakifanya mpaka litakaposomwa bungeni siku ya uwasilishaji bajeti ya serikali, na kwa sababu bado wiki mbili, niwaombe mkubali na muiamini serikali imepokea na inalifanyia kazi kwa uzito wake”.

“Mtakumbuka CCT mlikaa na Rais na mlipeleka ombi hili tayari Rais wetu alielekeza wataalamu walifanyie kazi, na tutakuja na taarifa wakati itakaposomwa bajeti ya serikali, lakini pia serikali ya awamu ya sita tayari imeshachukua hatua kwa baadhi ya mambo yanayohusiana na haya ikiwemo lile la misamaha ya kodi kwenye misaada”.