Chadema kutoshiriki uchaguzi Ngorongoro

Chadema kutoshiriki uchaguzi Ngorongoro

Muktasari:

  • Chadema imetangaza kutoshiriki uchaguzi mdogo wa jimbo la Ngorongoro huku iikionya watakaochukua fomu kwa jina la chama hicho.

  

Arusha. Chadema imetangaza kutoshiriki uchaguzi mdogo wa jimbo la Ngorongoro huku ikionya watakaochukua fomu kwa jina la chama hicho.

Uchaguzi huo unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, William Ole Nasha aliyefariki Septemba 27 jijini Dodomabaada ya kuugua kw amuda mfupi.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 28, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa amesema msimamo wa chama hicho bado ni kutoshiriki uchaguzi hadi kufanyika mabadiliko ya tume ya uchaguzi.

"Hatuna imani na Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) na huu ndio msimamo wetu, hivyo hatutashiriki uchaguzi wa jimbo la Ngorongoro, japo tunao wanachama wenye sifa ya kugombea," amesema Golugwa.

Amedai kuwapo watu walioandaliwa kwenda NEC kuchukuwa fomu, akisema: “Tutachukuwa hatua kali na tunataka jamii ijue hatutakuwa na mgombea Ngorongoro," amesema.

Katika uchaguzi Mkuu mwaka 2015 Chadema ilipata madiwani kadhaa katika jimbo hilo lakini hata hivyo baadaye walijiuzulu na kujiunga na CCM.

Hadi Sasa chama ambacho kinaendelea na mchakato wa kugombea jimbo hilo ni CCM ambao wagombea 17 walichukuwa fomu ndani ya chama hicho na wameshiriki kura za maoni.