Chadema wajibu hoja, Serikali ikiwaunga mkono kina Mdee

Muktasari:

Baada ya mawakili wa Halima Mdee na wenzake 18 kumaliza kuwasilisha hoja za kuomba ridhaa ya kufungua kesi kupinga wabunge hao kuvuliwa uanachama wa Chadema, mawakili wa chama hicho nao wamezijibu hoja hizo.

Dar es Salaam. Baada ya mawakili wa Halima Mdee na wenzake 18 kumaliza kuwasilisha hoja za kuomba ridhaa ya kufungua kesi kupinga wabunge hao kuvuliwa uanachama wa Chadema, mawakili wa chama hicho nao wamezijibu hoja hizo.

Leo Alhamisi Juni 30, 2020 mchana Jaji Mustapha Ismail katika Mahakama Kuu Masjala Kuu Dar es Salaam alianza kusikiliza sababu za Halima Mdee na wenzake 18 kuomba ridhaa ya kufungua kesi kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema.

Akijibu hoja hizo, kiongozi wa jopo la mawakili wa Chadema, Peter Kibatala japo alikubali kuwa kina Mdee wana maslahi na haki ya kuja mahakamani, lakini alipinga kuwa maombi yao yamefunguljwa nje ya muda.

Kibatala alidai kuwa kikomo cha muda kinahesabiwa kuanzia uamuzi wa awali wa Kamati Kuu ukiotolewa Novemba 27, 2020.

Katika kuunga mkono hoja yake hiyo, Kibatala aliwasilisha mahakamani uamuzi wa kesi mbalimbali zilizowahi kuamuriwa na Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na mahahakama za nje, ikiwemo Mahakama ya India.

Alifafanua kuwa mahakama hizo zilisema kuwa muda wa msingi wa kuleta maombi ya mapitio ya mahakama unaanza baada ya uamuzi unaolalamikiwa na kwamba kuwepo kwa rufaa mahakamani si kizuizi cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama.


Serikali yaunga mkono maombi ya kina Mdee


Serikali imeunga mkono maombi ya kina Mdee ya ridhaa ya kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama.

Kiongozi wa jopo la Makili wa Serikali wanaowakilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (wajibu maonbi), Stanley Kalokola alisema kuwa waombaji hao wametimiza vigezo vya kisheria vya kupata ridhaa hiyo.

Amevitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na muda wa kufungua maombi, baada ya uamuzi wanaotaka kuupinga akisema kwamba wamefungu maombi hayo ndani ya muda kwani maombi yanapaswa kufunguliwa ndani ya miezi sita tangu kutolewa kwa uamuzi unaopingwa kwani uamuzi unaopingwa ni wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 wakati maombi yamefunguliwa Juni 23, 2022.

Pia, Kalokola amesema kuwa kuna masuala ya kujadili waliyoyaibua waombaji yakiwemo madai ya kutokusikilizwa ambayo ni haki ya asili na ya Kikatiba na kwamba kama wanadai hivyo Mahakama inastahili kuwapa ridhaa hiyo ili iweze kuwasikiliza.

Pia Wakili Kalokola alisema kuwa ingawa Chadema si chombo cha umma kakini inafanya majukumu ya umma na hivyo ni sahihi kuomba mapitio ya Mahakama dhidi ya uamuzi wake.

Baada ya Jaji Ismail kusikiliza hoja za pande zote amepanga kutoa uamuzi Julai 6 mwaka huu.