Chadema wamlilia Profesa Baregu

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeeleza mchango wa mjumbe mstaafu wa kamati kuu ya chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumapili Juni 13, 2021.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeeleza mchango wa mjumbe mstaafu wa kamati kuu ya chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumapili Juni 13, 2021.

 Taarifa iliyotolewa leo na katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika inaeleza kuwa Profesa Baregu aliyefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),  alijipambanua katika kauli na matendo kupigania haki, utu, demokrasia  na heshima ya Mwafrika popote alipokuwa na alisimama mahiri katika hilo hadi umauti unamfika.

“Profesa Baregu ni miongoni mwa wanazuoni waliosimama imara kupigania mfumo wa vyama vingi nchini, kuuasisi na kuuishi wakati wote bila kuyumba akiamini pia katika hitaji la nchi la kupata Katiba Mpya itakayotokana na maoni ya wananchi wenyewe,” amesema Mnyika.

Pia ametoa salamu za pole kwa mke, watoto na  familia nzima ya  marehemu kwa kumpoteza baba, rafiki na nguzo ya familia.

“Tunatoa pole kwa Watanzania wote kwa kumpoteza mzalendo wa kweli na mpigania demokrasia mahiri, tunatoa pole kwa jamii ya wanazuoni wa Tanzania na Wanamajimui wa Afrika kwa kuondokewa na msomi mbobezi na mwana halisi wa Afrika,” amesema Mnyika.